24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TANROADS yajitosa kuwezesha Wakandarasi wa Kike

Na Sheila Katikula, Mwanza

Wanawake 80 kutoka Kanda ya Ziwa wameanza mafunzo ya ukandarasi wa barabara kwa kutumia teknolojia ya nguvu kazi ili kuwawezesha kujiajiri na kusimamia kwa ubora utunzaji wa miundombinu hiyo hapa nchini. 

Wanawake kutoka mikoa ya Geita, Kagera, Mara, Simiyu na Mwanza wakifundishwa namna bora ya ujazaji wa zabuni, taratibu za kusajili wa makampuni , sheria ya manunuzi, kanuni zake, namna ya kutumia mfumo wa manunuzi (TANePS) na usimamizi wa mikataba katika semina iliyosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS).

Akifungua Mafunzo hayo jana jijini Mwanza Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Mwanza Mhandisi Vedastus Maribe amesema kuwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inatekeleza sera ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika ujenzi na matengenezo ya barabara hapa nchini.

Maribe amewataka wanawake hao ambao wako katika hatua za awali za ukandarasi washiriki mafunzo hayo ya matengenezo na ukarabati wa barabara kwa kutumia teknolojia ya nguvu kazi kwa kuwa wasikivu ili waweze kupata uelewa wa kuwawezesha kufanya kazi zao vizuri.

Wanawake hao toka mikoa ya Geita, Kagera, Mara, Simiyu na Mwanza watafundishwa namna bora ya ujazaji wa zabuni, taratibu za kusajili wa makampuni, sheria ya manunuzi,  kanuni zake, namna ya kutumia mfumo wa manunuzi (TANePS) na Usimamizi wa mikataba.

“Mafunzo haya ambayo ni nadharia na kivitendo yatawawezesha kuwa tayari kusajili makampuni kwa wale ambao bado na hivyo kumudu soko la ushindani kwa kuomba kazi za ujenzi wa barabara kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa,” amesema Mhandisi Maribe.

Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake Wizara ya Ujenzi Mhandisi Liberatha Alphonce amesema kuwa lengo la kushirikisha wanawake hao wakandarasi  80 katika zoezi hilo ni kuhakikisha kuwa wanaunga mkono juhudi za serikali za uendelezaji na utunzaji wa miundombinu hapa nchini.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo zaidi na kuwapa ujuzi ili wanapofanya kazi za barabara wafanye kwa weledi na kwa mujibu wa sheria zilizopo, kufahamu namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa kazi za ukandarasi wa barabara.

“Mafunzo hayo ya wiki mbili yatahusu namna ya kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara kwa kutumia teknolojia ya nguvu kazi ili kuwawezesha kujiajiri na kukuza vipato vyao” alisema Mhandisi Alphonce.

Alisema kuwa wanawake hao wakandarasi watapa mafunzo yao kutoka kwa wizara ya ujenzi na uchukuzi, chuo cha Teknolojia ya ujenzi (ICOT) toka mkoani Mbeya,TANROADS, Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) na Bodi ya Usajili wa Wakandarsi (CRB). 

Naye mshiriki wa mafunzo hayo, Christina Macha toka mkoani Geita alisema kuwa mafunzo hayo yatampatia maarifa ya kiukandarasi na hivyo kumwezesha kufanya kazi hizo kwa weledi na kujiajiri.

Mshiriki toka mkoani Mara Mary Kiginga alisema kuwa anashukuru serikali kwa kutoa kipaumbele kwa kundi la wanawake katika kazi hizo za ukandarasi na hivyo kuondoa dhana potofu kuwa kazi hizo ni za wanaume .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles