*Yaeleza ilivyonufaika kupitia TADB
Na Nora Damian, Mtanzania Digital – Pwani
Kampuni ya Ufugaji Samaki ya Tanlapia inatarajia kuongeza uzalishaji kutoka tani 35 kwa mwezi hadi kufikia tani 100 ifikapo Juni 2025.
Kampuni hiyo imewekeza katika ufugaji samaki eneo la Kingami Kimarang’ombe Kata ya Nianjema Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Akizungumza Desemba 13,2024 wakati wa ziara ya waandishi wa habari waliotembelea mradi huo
Meneja Uzalishaji wa Kampuni ya Tanlapia, Farida Buzohera, amesema Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) iliwapatia mkopo uliowezesha ujenzi wa miundombinu ya mradi huo.
“TADB wametusaidia sana mpaka hapa tulipofika, tunawashukuru kwa juhudi zao wametusaidia hasa katika ujenzi wa miundombinu. Hadi sasa tuna miaka minne na tunazalisha wastani wa tani 35 za samaki kwa mwezi, tunatarajia hadi Juni 2025 tufikie tani 100 kwa mwezi,” amesema Buzohera.
Kwa mujibu wa meneja huyo, wana ekari 650 na malengo ni kuongeza uzalishaji kukidhi mahitaji ya kitoweo hicho nchini.
Naye Meneja wa TADB Kanda ya Mashariki, Michael Madundo, amesema kwa kutambua umuhimu wa sekta hiyo wanatekeleza mikakati ya kuwawezesha wafugaji samaki ili kuongeza uzalishaji nchini.
Amesema mradi wa Tanlapia ni wa kimkakati na kwamba wanajivunia kuuwezesha hadi kufikia hatua ya sasa ya kuzalisha tani 35 kwa mwezi kutoka tani 5.
“Tunajivunia mradi huu kwa sababu unasaidia kutekeleza mikakati na malengo ya Serikali kwa kuongeza utoshelevu wa chakula nchini na umetengeneza ajira za kutosha. Mpaka sasa umeajiri wafanyakazi 116, kati yao 88 wanafanya kazi za vipindi kulingana na mahitaji yanayotokea na 28 ni wa kudumu.
“Pia tunajivunia kwa sababu umeweza kuajiri vijana na kinamama ambao wako 47 mpaka sasa, mradi unavyoendelea kukua tunategemea ajira zitaongezeka zaidi na wananchi hasa wa Bagamoyo watazidi kuongeza vipato vyao kupitia mradi huu,” amesema Madundo.
Amesema benki hiyo ina mkakati wa kufikia malengo ya Serikali ya kuhakikisha kunakuwa na utoshelevu wa samaki nchini.
Takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinaonyesha hadi kufikia Aprili 2024 uzalishaji wa mazao ya ukuzaji viumbe maji umefikia tani 43,415.95 kutoka tani 33,525.46 za mwaka 2022/2023 huku ukijumuisha tani 34,825.5 za samaki.
Uzalishaji huo umewezesha familia kupata kipato pamoja na kuongeza usalama wa chakula na lishe kwa kuchangia asilimia 30 ya protini inayotokana na wanyama huku ikikadiriwa kwamba kwa wastani kila Mtanzania anakula kilo 7.9 kwa mwaka.