Bakari Kimwanga -ARUSHA
SERIKALI kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa umeme kuunganisha Tanzania na Kenya unaojulikana kama Kenya-Tanzania Power Interconnection (KTIPIP).
Hatua hiyo ni utekelezaji wa mradi huo wa awamu ya kwanza ya kuziunganisha nchi zilizopakana na Tanzania kuwa na umeme wa uhakika huku awamu ya pili ya mradi huo ukihusisha nchi za Tanzania na Zambia (ZTK) ambao nao tayari umeanza kutekelezwa ambapo kazi ya kutengeneza misingi ya kusimika minara imeanza.
Akizungumza leo Januari 23 katika kijiji cha Nanja wilayani Monduli mkoani Arusha, unapojengwa mradi huo. Mratibu wa mradi huo kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Peter Kigadye, amesema kuwa mradi huo ni sehemu moja ya mradi mzima wa Regional Power Connection ambao lengo lake ni kuunganisha mfumo wa umeme wa Tanzania na Afrika Mashariki (East Africa Power Pool) kwa upande wa Kaskazini.
Amesema baada ya kukamilika utekelezaji wake sehemu nyingine ya tatu inayounganisha mifumo ya nchi Kusini mwa Afrika, kupitia mradi wa Southern Africa Power Pool (SAPP)
“Tanzaania tumebarikiwa tutakuwa na sehemu tatu ya kwanza ni mradi wa Backborn ambao umejengwa katikati ya nchi yetu na ulikuwa na kilomita 670 inaanzia Shinyanga hadi Iringa.
“Sehemu ya pili ni kuunga kutoka Singida hadi mpakani na Kenya ambapo kuna kituo kimoja kinachoitwa Isinya, jumla mradi huo wote una umbali wa kilomita 510 ambapo kwa Tanzania zipo kilometa 414 na upande wa Kenya kuna kilometa 96 na hizo ndio kilomita za mradi tunazoanza kuutekeleza hivi sasa.
“Baada ya hapo sehemu ya tatu ni kuanzia Iringa kwenda Kusini ambapo kuna mradi utakaoitwa Zambia Interconector ambako kuna kilomita nyingine 624 kwa hiyo Tanzania tutakuwa tumekamilisha ule mkongo wa msongo wa Kilovoti 400,” amesema. Mhandisi Kigadye
Akifafanua zaidi kuhusu kuunganiushwa kwa umeme kwenye nchi za Ukanda wa Mashariki na Kusini, amesema kuwa lengo ni kuiunganisha Tanzania ili kuleta ufanisi na kuwa na umeme wa uhakika.
Amesema mradi mzima una urefu wa kilomita 510 na umegawanyika kwenye sehemu nne, ambazo ni Isinya Kenya hadi Namanga Kilomita kilomita 96, sehemu ya pili unahusu Namanga-Arusha Kilomita 114, sehemu ya tatu Arusha-Babati kilomita 150, na Bababti-Singida kilomita 150.
Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Tanesco anayehusika na miradi, Mhandisi Emmanuel Manirabona, amesema tayari vifaa vya kutekeleza ujenzi wa mradi huo vimewasili kwa kiasi kikubwa cha kazi kuanza.
Mhandisi Manirabona, amesema kuwa kila kitu kiko sawa na wananchi wote ambao wako kwenye sehemu mradi unakopita, tayari Serikali imeshawalipa fidia na ndiyo maana mkandarasi anaendelea na kazi.
Amesema gharama za mradi huo zinatokana na mkopo uliotolewa na Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (ADB), JICA pamoja na Serikali ya Tanzania ambao umegharimu dola za Marekani milioni 258.