Tanesco yatakiwa kutengeneza mfumo kuhudumia wateja kwa wakati

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital 

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amekitaka kituo cha huduma kwa wateja cha Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), kuandaa mkakati na mfumo utakaosaidia kuwahudumia wateja wote wanapiga simu kwa wakati.

Hayo ameyasema Novemba 27,2023 jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea kituo hicho ili kuona utendaji kazi wa kituo na majukumu yake.

Amesema kumekuwa na mapungufu mengi katika shirika hilo ikiwamo upande wa huduma kwa mteja, kwani kwa siku zinapigwa simu 40,000 na zinazopokelewa ni simu 12,000 pekee.

“Nimewaelekeze kitengo cha huduma kwa wateja Tanesco wahakikishe ndani ya muda mfupi waje na mikakati ambayo itawafanya wateja wote waweze kusikilizwa na changamoto zao kutatuliwa kwa wakati,”amesema Kapinga.

Amesema kuna changamoto ambazo ni sugu kwenye shirikika hilo zinapaswa kutatuliwa kwa haraka ili kuendana na kasi ya teknolojia iliyopo.

Amesema changamoto zinaposhindwa kupatiwa suluhu kuna mambo mawili aidha shirika limeshindwa au waliopewa jukumu hilo wameshindwa, hivyo itailazimu serikali kutafuta wengine kwani kwa karne hii swala la huduma kwa mteja halipaswi kuwa kikwazo.

Amesema pamoja na kuwa na changamoto ya umeme lakini mteja hapaswi kuwa na mawazo kwa ajili ya kushindwa kusikilizwa, kwani mtu anapopata changamoto anapaswa kutatulia kwa muda wa saa tatu mpaka nne.

“Kwa takwimu za sasa hivi asilimia 32 wanahudumiwa kati ya saa tatu mpaka nne lakini asilimia 52 wanahudumiwa  ndani ya saa nane, niwaambie tu tulipofikia sasa umeme sio anasa umeme ni swala la msingi kwa kila mtanzania huwezi kumuacha mteja saa12 hana umeme kwa sababu umeshindwa kwenda kumtatulia changamoto yake,mgao ni kitu kingine na kumtatulia mteja changamoto yake ni jambo lingine,”amesisitiza.

Aidha amewataka kuhakikisha wanawalipa stahiki zao wafanyakazi wote wa kituo hicho ili waendelee kutoa huduma bora na stahiki kwa mteja, huku wakitambua kuwa mteja ni mfalme hivyo wanapaswa kuhudumiwa kwa nidhamu.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kituo hicho,  Martine Mwambene amesema wamepokea maelekezo yote na watayafanyia kazi kwa wakati.

“Tumepokea maelekezo na tutayanyia kazi kwani tayari tumeshaanza kuandaa mitandao mbalimbali ambayo tunaweza kuwasiliana na mteja ikiwemo mitandao ya kijamii lakini pia kwa kutumi ssd cord,”amesema Mwambene.