23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Tanesco yaja na maboresho mita za Luku, wateja wapewa tahadhari

Na Mwandishi wetu, Mwanza

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linatarajia kuanza maboresho ya mfumo wa mita za Luku kuanzia Juni Mosi hadi Novemba 24, mwaka huu, ili kuziongezea ufanisi na usalama, na kuendana na mabadiliko ya viwango vya mita za Luku za kimataifa.

Maboresho hayo ambayo ni matakwa ya shirika la kimataifa la viwango vya Luku hufanyika kila baada ya miaka 10, ambapo Juni mosi, mwaka huu yataanzia kwa wateja wa mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu, Geita, Katavi, Shinyanga na Tabora.

Akizungumzia maboresho hayo, Kaimu Mkurugenzi wa mawasiliano na uhusiano kwa umma –Tanesco, Irine Gowelle, amesema kuwa kuanzia jumamosi mteja atakayenunua umeme atapata tokeni zenye namba 60 zikiwa katika makundi matatu (kundi la kwanza na la pili yatahusu maboresho), atakapozijaza atakuwa tayari ameiboresha mita yake.

Amewataka wateja ambao hununua umeme wa ziada kuhakikisha kuwa kabla ya kufanya maboresho hayo wajaze umeme huo kwani wasipofanya hivyo watakuwa wameupoteza.

“Zoezi hili ni jepesi na ni la mara moja tu wateja wetu watusaidie ili tukamilishe. Tulianza zoezi hili Kigoma sasa ni zamu ya mikoa hii tuliyoitaja, baada ya hapa tutakuwa tukielekea katika mikoa mingine kwa awamu.

“Niwaombe wakazi wa mikoa ambao tunaanza maboresho Juni mosi watoe ushirikiano ili tuweze kufanikisha kuendana na viwango vya Luku vya kimataifa na kuleta ufanisi katika huduma ya Luku nchini,” ameongeza:

“Wateja wasipofanya maboresho katika kipindi hicho, mteja hataweza kununua umeme wala kupata umeme na itamlazimu atutafute tumfanyie mabadiliko hayo ili aendelee kupata huduma ya umeme,” amesema Kaimu Mkurugenzi huyo.

Katika hatua nyingine, shirika hilo limeonya vitendo vya wizi wa mita za Luku ambao umeshamiri mkoani Mwanza, kwani litawachukulia hatua kali huku likiahidi kufanya uchunguzi kama kuna watumishi wanaoshiriki katika wizi huo.

“Baada ya kufanya ukaguzi wetu wa ndani tumebaini mita za Luku zinaibwa mpaka sasa takribani mita 1,000 zimeripotiwa kuibwa, baadhi ya watuhumiwa tumewafikisha katika vyombo vya kisheria na wengine tunaendelea kuwachukulia hatua na kuwabaini,” amesema Gowelle na kuongeza:

“Tunawaomba wateja wetu wawe makini usiruhusu kufungiwa mita ambayo siyo ya kwako, wawe walinzi wa mita hizo na kutoa taarifa kwenye shirika ili kuepusha kuhujumu miundombinu ya shirika na kukwamishwa jitihada za kuleta ufanisi katika utuoaji wa huduma,” ameongeza Gowelle.

“Tuna zoezi la kupima uridhikaji wa huduma zetu kwa wateja, kwahiyo niwaombe wateja wetu utakapokutana na dodoso hilo usisite kutupa maoni yako namna gani tunaweza kufanya maboresho ya huduma zetu. Pia watakaopata changamoto wakati wa zoezi hili la maboresho wawasiliane na sisi,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles