TANESCO WAWAKAMATA WEZI WA UMEME

0
1134

Na JANETH MUSHI, ARUSHA


 

pinguMAOFISA wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Mkoa wa Arusha, wamefanya msako wa wezi usiku wa manane katika maeneo mbalimbali jijini hapa.

Katika msako huo, askari hao wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 15 waliokuwa wameunganishiwa umeme kinyume na taratibu.

Akizungumza baada ya operesheni hiyo, mdhibiti wa mapato wa shirika hilo mkoani hapa, Hassan Juma, alisema katika maeneo mbalimbali waligundua nyumba zaidi ya 100 zimeunganishwa umeme huo wa wizi.

“Katika operesheni hiyo tuliyoifanya katika maeneo mbalimbali yakiwamo katika Kata ya Ngarenaro, tulibaini watu wengi wanatumia umeme wa wizi jambo ambalo linasababisha hasara kubwa.

“Kibaya zaidi, watu hao wameunganisha umeme wao katika mazingira hatarishi, jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha yao wakati wowote.

“Kwa kifupi katika operesheni ile, tumefanikiwa kukamata watuhumiwa 15 ila bado tunaendelea na msako wa watuhumiwa wengine kwani tumebaini nyumba zaidi ya 100 zimeunganishiwa umeme wa wizi,” alisema Juma.

Kwa upande wake, Ofisa Mahusiano Huduma kwa Wateja mkoani hapa, Fredy Robert, alisema walilazimika kufanya msako huo usiku wa manane ili kuweza kudhibiti wizi huo.

“Tulilazimika kutembea usiku kwa sababu mchana watuhumiwa wengi wamekuwa wakikimbia, hivyo tukaona njia sahihi ya kuwakamata ni kuwatembelea usiku,” alisema Juma.

Baadhi ya watuhumiwa hao waliokamatwa katika Kata ya Ngarenaro walikiri kutumia umeme kwa njia ya wizi na kudai wameunganishiwa na watu waliojitambulisha kwao kuwa ni maofisa wa Tanesco.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here