26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

TANESCO kuwajengea uwezo wahandisi wanawake

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Kutokana na uhaba wa wahandisi wanawake, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limezindua programu maalumu ya kuwajengea uwezo wahandisi wanawake kwa kuwaendeleza kiujuzi na kielimu lengo likiwa kuongeza ushiriki wao katika shughuli za uendelezaji miradi ya umeme nchini.

Akizungumza jana Januari 29,2024 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa programu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gisima Nyamo_Hanga amesema mpango huo ni wa miaka minne na watashirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT),ambavyo watavitumia kuwaendeleza kielimu wataalamu wa kike wa shirika hilo na kuwapata wanafunzi wanaohitimu fani ya uhandisi.

“Ushiriki wa wahandisi wanawake bado ni mdogo hususani katika sekta ya umeme na sisi kama TANESCO tumeona ni muhimu kuja na mkakati maalumu ambao utasaidia kuongeza wahandisi wengi wa kike ambao tutawaajiri na kufanya nao kazi.

“Mradi huu unaratibiwa na Umoja wa Ulaya, lakini mpango wetu wa mbele ni kuhakikisha kwamba unakua endelevu na hata baada ya huu mradi kuisha sisi wenyewe tuweze kuendelea, lengo ni kuwapata wahandisi wengi wanawake ,”amesema Mhandisi Nyamo-hanga.

Ameongeza kuwa, mradi huo umeanza na wanawake 40, huku akitoa rai kwa wahandisi wakike kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mpango huo.

“Mradi huo ni moja ya kichocheo cha kuwahamasisha watoto wakike kusoma fani ya uhandisi, tumeanza na wanawake 40 lakini kila mwaka tutakua tunaongeza wengine,”amesema.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dk. Seif Shekalage, amesema programu hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wanawake wanaendelezwa kiuchumi, kielimu na kuongeza usawa wa kijinsia.

Amesema wizara hiyo ipo tayari kushirikiana na TANESCO ili programu hiyo iwe mfano bora wa kuigwa na taasisi na mashirika mengine nchini.

“Serikali itaendelea kushirikiana na TANESCO ili kuhakikisha idadi ya wanawake katika shirika inaongezeka mpaka kufikia 2026,”amesema Shekalage.

Kwa upande wake mnufaika wa programu hiyo Mhandisi Catherine Mwigoha kutoka TANESCO,amesema kupitia mradi huo utasaidia kuwaongezea ujuzi ambao utawezesha kuongezeka kwa uzalishaji ndani ya shirika hilo.

Ameongeza kuwa mradi huo utawasaidia kupata fursa ya kushika nafasi mbalimbali za maamuzi na kuongeza uzoefu wa kupata nafasi za ajira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles