Na Upendo Mosha-MOSHI |
KATIKA kile kinachoelezwa kudhibiti madeni sugu ya umeme kwa idara na taasisi za Serikali, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Kilimanjaro, limeanza kazi ya kufunga mita za malipo ya awali (LUKU).
Taasisi ambazo zinafungiwa mita hizo ni zile zinazodaiwa madeni ya zaidi ya Sh bilioni tatu kwa vile hatua hiyo itawasaidia kutumia huduma ya umeme kulingana na matumizi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Mahawa Mkaka, alisema shirika hilo limefikia uamuzi huo kudhibiti kuongezeka malimbikizo ya ankara za umeme kwa taasisi hizo.
Alisema shirika hilo limefanya mazungumzo na baadhi ya taasisi za serikali zinazodaiwa malimbikizo makubwa ya ankara za umeme na kukubaliana kuwafungia mita za malipo ya awali waweze kuendelea kupata huduma ya umeme huku wakilipa madeni yao.
“Kuanzia sasa tumekubaliana shirika litawafungia mita za malipo ya awali mashirikia yote ya umma na madeni yao watayalipa kulingana na makubaliano yetu.
“Tunaamini suala hii itakuwa ndiyo njia pekee ya kumaliza madeni yao na kutoongezeka madeni,” alisema Mkaka
Alitumia fursa hiyo kutangaza kwamba Tanesco limesitisha rasmi kukata umeme katika tasisi za serikali ambazo ni Jeshi la Polisi na Magereza kutokana na kuwapo makubaliano maalumu.
“Jeshi la polisi na magereza hatutawakatia umeme ndani ya gereza wala kituo cha polisi ila katika nyumba za polisi na askari magereza kila mtu atalazimika kujilipia bili zake za umeme kwa kutumia mita za luku tofauti na ilivyokuwa awali,” alisema Mkaka.
Alisema kazi hiyo itakwenda pamoja na operesheni ya kusimamisha umeme kwa baadhi ya taasisi za serikali ambazo zimeshindwa kufikia makubaliano na shirika hilo ya kufungiwa mita za luku na kulipa malimbikizo ya madeni yao.