Grace Shitundu-DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), inajivunia mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli na kusema kuwa imeweza kutanua wigo wa hifadhi na kukuza sekta ya utalii nchini.
Pamoja na hayo Tanapa imeimarisha utalii na imefanikiwa kukusanya mapato na kuchangia pato la taifa kwa asilimia 17.5 kwa mwaka na asilimia 25 ya fedha za kigeni nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa, Dk. Allan Kijazi, alisema kuwa mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka minne yanatokana na juhudi za Serikali ya awamu ya tano za kutangaza utalii ndani na nje ya nchi.
Dk. Kijazi alisema kuwepo kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kuimarishwa kwa miundombinu ya ndani ya hifadhi na nje pamoja na viwanja vya ndege, ni sehemu mojawapo ya kuimarisha na kuvutia idadi kubwa ya watalii ambao kwa sasa wanakuja nchini.
“Na ukiangalia utalii unaofanyika nchini, sehemu kubwa ni katika hifadhi za taifa, takwimu zinaonyesha nusu ya watalii wanatembelea hifadhi za taifa,” alisema Dk. Kijazi.
Alisema katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano watalii wa ndani na nje wameongezeka kutoka wastani wa 700. 19 kwa mwaka 2015/16 hadi kufikia milioni 1.1 ambayo ni zaidi ya asilimia 70.
“Idadi hii haiongezi tu mapato, bali pia inaongeza ajira. Katika kipindi cha miaka minne Tanapa wamefanikiwa kuongeza ajira 750,000 na takwimu inaonyesha Watanzania zaidi 100,000 wameajiriwa katika sekta ya utalii kutokana na kuongezeka wawekezaji na wengine kujiajiri wenyewe,” alisema Dk. Kijazi.
Alisema mwaka wa fedha 2015/16 wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani walikuwa wanakusanya Sh bilioni 175, lakini 2018/19 wamekusanya Sh bilioni 279. Kumekuwa na ongezeko la Sh bilioni 100 katika kipindi cha miaka minne.
“Mchango wa Tanapa katika Mfuko Mkuu wa Serikali umeongezeka. 2015 mchango ulikuwa Sh bilioni 3.5, lakini mwaka wa fedha uliopita umekuwa Sh bilioni 42. Hili ni gawio linalokwenda moja kwa moja serikalini, lakini kuna kodi mbalimbali ambazo Tanapa tunalipa.
“Katika kipindi cha miaka minne tumewekeza kiasi cha Sh bilioni 111 kuimarisha miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na makazi katika hifadhi,” alisema Dk. Kijazi.
Alisema pia wameimarisha ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki, iliyounganishwa na mifumo ya Serikali na kuondokana na kufanya malipo kwa hundi au fedha taslimu, hivyo kupunguza mianya ya upotevu wa fedha.
Dk. Kijazi alisema kiuhifadhi ukubwa wa eneo ndio muhimu zaidi kiikolojia na awamu hii ya tano imevunja rekodi ya kuanzisha maeneo makubwa ya kuuhifadhi ukilinganisha na awamu zilizopita.
Alisema kipindi cha ukoloni kulikuwa na hifadhi tatu tu zenye ukubwa wa kilomita za mraba 17,000 na baada ya uhuru hadi awamu ya nne kulikuwa na hifadhi 16 jumla zilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 57,000.
“Lakini awamu ya tano zimeanzishwa hifadhi mpya tatu, ile ya Burigi Chato, Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagwe na nyingine tatu zinazotarajiwa ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere (zamani Selous Game Reserve), Kigosi Kahama na Hifadhi ya Taifa ya Ugara ambazo zote zitakuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 47,000 na kufanya eneo lote la hifadhi 22 kuwa na kilomita za mraba 100,004,” alisema Dk. Kijazi.