MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Meck Sadiki, amemaliza minong’ono ya wanasiasa waliokuwa wakishinikiza kurejeshwa kwa eneo la ukanda wa Nusumaili, ambalo ni hifadhi ya msitu wa Mlima Kilimanjaro kwa wananchi na kusema kuwa msimamo wa Serikali ni kulinda na kuhifadhi eneo hilo na si vinginevyo.
Mkuu huyo wa mkoa aliyasema hayo jana katika hafla fupi ya kukabidhi jengo la bwalo la chakula katika shule ya Sekondari ya Mwika iliyopo wilayani Moshi ambapo ujenzi wake umefadhiliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).
RC Sadiki alisema wapo baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakiishinikiza Serikali kurejesha eneo hilo kwa wananchi wa vijiji wanaozunguka katika hifadhi hiyo kwa lengo la kujipatia mahitaji yao ya kibinadamu, jambo ambalo alidai ni kuhatarisha usalama na uhifadhi wa mazingira ya Mlima Kilimanjaro.
“Licha ya jitihada zinazofanywa na Tanapa za kuhakikisha hifadhi zetu zinakuwa salama kwa ustawi wa uchumi wetu, bado kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wanasiasa kukwamisha jitihada hizo, sasa msimamo wa Serikali ni kwamba eneo la Nusumaili halitarejeshwa kwa wananchi, litabaki chini ya usimamizi wa hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa),” alisema Sadiki.
Alisema eneo hilo la ukanda wa Nusumaili lina ukubwa wa kilomita za mraba 51.2 na kwamba lilikabidhiwa kwa Tanapa mwaka 2005 kwa lengo la kulihifadhi kutokana na hapo awali kumilikiwa na taasisi mbalimbali na kushindwa kulisimamia ipasavyo, hali iliyochangia wananchi kuvuna mazao mengi ya misitu kiholela na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Awali akizungumza wakati akikabidhi jengo hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi, alisema ujenzi huo umegharimu jumla ya Sh milioni 186.4 ambapo shirika hilo limechangia Sh milioni 126, wananchi milioni 10 na Halmashauri ya wilaya ya Moshi milioni 49.5.