Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
CHAMA cha Wamiliki wa Malori Wadogo na Wakati Tanzania(TAMSTOA), wameiomba Serikali kushughulikia changamoto zinazowakabili hasa kamatakamata ya magari na ufinyu wa barabara.
Akizungumza katika Mkutano wa tano wa mwaka 2024 wa chama hicho uliofanyika leo Februari 5, 2025, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TAMSTOA, Shaban Chuki, amesema kuna changamoto nyingi wanakutana nazo ikiwamo pia suala la ushuru wanaotozwa na Mamlaka ya Mapato nchini(TRA).
Mwenyekiti huyo amesema ombi lake kwa Serikali kwa niaba ya wanachama wenzake, ni kusaidiwa kuondoa kero zinazowakabili na kujengewa barabara hata ya vumbi katika maeneo ambayo barabara ni ndogo na malori yanapita mengi.

Amesema barabara ya kutoka bandarini kuelekea barabara ya Morogoro imekuwa ni finyu, viongozi watambue kuwa magari yamekuwa yakiongezeka kila siku lakini miundombinu bado imebaki ya zamani katika baadhi ya maeneo.
Ameitaja sehemu inayowapa kero zaidi kwa upande wa Dar es Salaam ni Wilaya za Temeke na Ubungo kutokana na ukamataji wa malori unaokuwepo maeneo hayo bila kujali kuwa inasababishwa hali ya kukosa sehemu sahihi za kupaki.
TAMSTOA imeomba pia kuangaliwa kwa utaratibu wa utozwaji wa ushuru katika eneo la Mikumi, Morogoro kwani limekuwa likiwaumiza.
“Magari yote yanayobeba mizigo kutoka nje ya nchi yanategemea bandari ya Dar es Salaam na hasa wilaya ya Temeke. Naomba Viongozi wa Temeke watambue ongezeko la malori ni fursa na neema na si karaha, imegeuzwa sasa hivi kuona malori kuwepo ni karaha, licha ya kuchangia pato la Taifa kutengeneza hizi barabara lakini hatuthaminiwi.
“Ninaomba tukae pamoja tupange tuoneshwe ni wapi tunatakiwa kubaki, wapite kwa utaratibu upi? Na tufahamu kuwa si wote wanaokuja kuchukua mizigo bandarini sio wote wana sehemu maalumu ya kupaki,” amesema Chuki.
Ameeleza kuwa vitendo vya kukamatwa bila utaratibu vimekuwa ni changamoto kubwa kwao kutokana na kusababisha uwepo wa vibaka na vishoka wanaotaka fedha kutoka kwa madereva.
Kutokana na hilo wameiomba Serikali kuwatafutia eneo maalumu la kubaki malori na kuitaka TRA kutembelea wasafirishaji na kuacha kamatakama eneo la Mikumi mkoani Morogoro ambako kumekuwa ni chanzo cha rushwa.
“Katika kipindi cha mwaka 2024 tumeweza kutatua changamoto kamatakamata malori wilayani Temeke na Ubungo mkoani Dar es Salaam, japo bado tatizo halijaisha. Tunaionba Serikali ifanyie kazi,” amesema Chuki.
Akitoa taarifa ya chama tangu kuanzishwa kwake amesema kimefikisha jumla ya wanachama 900 ambao wanamiliki zaidi ya malori 26,000.
Amesema uwepo wa malori hayo umeweza kutoa ajira kwa watanzania 52,000 ambao ni madereva na wasaidizi.
Aidha ameeleza kuwa malori hayo 26,000 yakipata
Ameeleza kuwa lengo la TAMSTOA ni kusimamia na kutatua changamoto inayohusisha sekta ya usafirisha kwa njia ya barabara pamoja na kutetea maslahi ya wanachama kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania.
Pia kuhamasisha wamiliki wa malori kutoa mikataba madereva kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi na Ajira, ikiwamo kuhakikisha kunakuwa na mazingira rafiki ya biashara ya usafirishaji ili kuongeza pato la Taifa.
Aidha amesema malori yanayomilikiwa na wanachama hao, yakipata mzigo kwa wakati mmoja yanatumia zaidi ya lita milioni 62.4 za mafuta, zinazogharimu zaidi ya sh. milioni 187 kwa siku kwa mwaka ikiwa ni zaidi ya sh trilioni mbili.
“Kwa takwimu hizo ni wazi kuwa sekta ya usafiri ina mchango mkubwa kwenye pato la Taifa na jamii kwa ujumla.
Kuhusu vita ya DR Congo, Mwenyekiti huyo amesema wanaishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuwaokoa madereva wote walikuwa katika Mji wa Goma.
Kwa upande wake mwakilishi wa mgeni rasmi katika mkutano huo, Geoffrey Silanda aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, amesema TAMSTOA imekuwa na utaratibu wakufanya mkutano kuzungumzia mafanikio na changamoto zao na wamekuwa wakishirikiana.
Silanda amesema kwa niaba ya Serikali kupitia wizara ya Uchukuzi, wamekuwa wakishirikiana kutatua changamoto mbalimbali ikiwamo suala la upimaji wa mizigo katika mizani ambalo linatafutiwa ufumbuzi pamoja na ukamataji wa eneo la mikumi.
“Kweli kumekuwa na changamoto katika maeneo ya maegesho hapa nchini, TANROADS imeelelzwa kutafuta maeneo mbadala ya maegesho yatayoondoa changamoto hiyo”, amesema.
Naye Mkaguzi wa Polisi kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani Makao Makuu, Dumu Mwalugenge amesema katika kuzuia ajali za barabarani wanashirikiana na chama hicho kwa kutoa elimu kwa madereva na kuhakikisha foleni zinaondoka ili kuwapunguzia wamiliki gharama za uendeshaji.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kufanya tathimini ya kile walichokifanya katika kipindi cha miaka 10 tangu chama hicho kilipoanzishwa mwaka 2014 ambapo miongoni mwa mambo waliyofanya ni kuhamasisha wamiliki wa Malori kutoa mikataba kwa madereva.
Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Kulinda na kutetea maslahi ya wanachama.Ubunifu na kuinua wamiliki wa malori wadogo na wa kati hadi viwango vikubwa. Kushirikiana na Serikali kutatua changamoto za sekta ya usafirishaji,”