29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

Tamati mifuko ya plastiki

Waandishi Wetu -DAR/MIKOANI

LEO ni siku ya mwisho ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini, changamoto iliyobaki ni namna mamlaka za chini zitakavyotekeleza mwongozo uliotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Tayari mikoa mbalimbali imetoa matamko ya namna itakavyotekeleza amri hiyo ya kuhakikisha mifuko hiyo haitumiki tena.

Mwongozo kwa wakaguzi na watekelezaji wa katazo la mifuko hiyo, unaelekeza kuwa ukaguzi utafanyika madukani, magengeni, sokoni, katika maduka makubwa, ghalani, viwandani na kwenye maeneo mengine zinakouzwa bidhaa.

“Wakati wowote wa ukaguzi wajitambulishe na kuonesha vitambulisho vyao kwa wahusika kwenye maeneo wanayoyakagua, hairuhusiwi kumsimamisha mtu na kumpekua au kupekua mizigo yake ili kutafuta mifuko ya plastiki,” inaeleza sehemu ya mwongozo huo.

Pia hairuhusiwi kuingia kwenye makazi ya watu au kusimamisha magari au vyombo vingine vya usafiri ili kutafuta mifuko ya plastiki, iwapo vitasimamishwa kwa sababu nyinginezo na kukutwa na mifuko hiyo, adhabu stahiki itatolewa kwa wahusika na wataelekezwa mahala pa kupeleka shehena hiyo.

Atakayekutwa na kosa la kuendelea kuuza, kuhifadhi na kutumia mifuko hiyo ataelekezwa pa kuipeleka, atapigwa faini na atasainishwa fomu kukubali faini hiyo na atapewa muda wa kulipa.

“Atakapokataa kusaini au kushindwa kulipa katika muda aliopewa, ndipo atafunguliwa mashtaka. Watakaotozwa na kulipa faini watapewa risiti za Serikali kwa malipo yao.

MKANGANYINGIKO

Wakati mwongozo huo ukisema hayo, mkoani Mwanza watekelezaji wa katazo hilo pamoja na majukumu mengine, wametakiwa kuingia kwenye jengo lolote, gari, ndege, chombo cha majini na mahali pengine popote pasipo na makazi ya watu na kufanya ukaguzi.

Wakati mwongozo ukipinga kusimamisha magari kwa ajili ya ukaguzi, watekelezaji hao wa sheria hiyo mkoani Mwanza wametakiwa kusimamisha  gari au chombo chochote cha majini au ardhini na kufanya ukaguzi, kupiga picha za video na kawaida, kuchukua sampuli, kuandika kumbukumbu au kutoa nakala za taarifa kwa kutumia mbinu yoyote.

Akikabidhi vitambulisho kwa wakaguzi wa mkoa huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole,  alisema vimetolewa kufuatia kifungu cha 183(2) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Baraza  la Usimamizi wa Mazingira .

Alisema vitambulisho hivyo vilitengenezwa ofisi ya Makamu wa Rais kwa ajili ya maofisa 23 wa Mkoa wa Mwanza  walioshiriki mafunzo ya wakaguzi wa mazingira ili waweze kushiriki kwa ukamilifu kwenye usimamizi na  ufuatiliaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki.

 “Zoezi hili ni la kisheria, kama mkoa hatutaki kusikia linafanyika tofauti na mikoa mingine maana maelekezo ni yaleyale na yametolewa na mtu mmoja ambaye ni Makamu wa Rais, hatuhitaji kusikia kero au mgogoro wowote, kila mmoja afuate sheria,” alisema.

ARUSHA MAHABUSU ZIKIJAA, WATUHUMIWA KUFUNGIWA UWANJANI

Mkoani Arusha, polisi wamesema endapo mahabusu zote zitajaa, watuhumiwa wa mifuko ya plastiki kabla ya kuwapeleka mahakamani watawafungia ndani ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Akisisitiza utii wa sheria bila shurti, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha (RPC), Jonathan Shanna alisema wanaendelea na jaramba la kukabiliana na watakaokaidi maagizo ya Serikali.

 “Tumeanza mazoezi ya kuwakamata na kuwaweka mahabusu watakaomatwa wamekaidi maagizo ya Serikali. Wapo baadhi ya watu wanaowakejeli wakidai mahabusu tutawaweka wapi.

 “Nataka niwaambie, siku zote mahabusu hazijai, wakijaa kwenye chumba tutahamishia chumba kingine, nacho kikijaa tutawahamishia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, maana ya mahabusu ni kuwa chini ya ulinzi wa polisi.

 “Tutawalinda usiku na mchana pale uwanjani, hiyo ndiyo kazi yetu kusimamia na kuona watu wakitii sheria bila shuruti, wakitoka pale ni papaa mahakamani, papaa jela,” alisema RPC Shanna.

Alisema jeshi hilo litahakikisha linasimamia sheria na maagizo yaliyotolewa na Serikali kwa kuwakamata wale wote watakaoendelea kukaidi na kuvunja sheria.

 “Niwaombe wakazi wa Mkoa wa Arusha wasing’ang’ane kupata tabu wala shida kwa kukaidi na kuendelea kutumia mifuko ya plastiki,” alisema.

DAR MIFUKO YAANZA KUPOTEA

Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam, baadhi ya maeneo mifuko hiyo imeanza kutoweka.

MTANZANIA lilitembelea katika masoko ya Kariakoo na Mchikichini ambalo ni maarufu kwa kuuza nguo na viatu vya mtumba na kushuhudia wafanyabiashara na watu waliokwenda kutafuta bidhaa katika masoko hayo wakiwa na mifuko mbadala.

Wamachinga ambao mara nyingi walikuwa wakitembeza mifuko ya plastiki, jana walionekana wakiuza mifuko mbadala.    

Mwenyekiti wa Chama cha Wamachinga Kariakoo (KAWASSO), Stephen Lusinde, alisema wanazingatia na kutekeleza maelekezo yanayotolewa na Serikali na tayari wameanza kutoa elimu kwa wanachama wao.

“Chama chetu kina wajumbe 47 ambao tumewaelekeza wanapita katika kila mitaa ya sokoni Kariakoo kufikisha ujumbe kwa wadau wetu, kwamba wapokee maelekezo ya Serikali mifuko ya plastiki haitakiwi,” alisema Lusinde.

Wafanyabiashara kadhaa waliozungumza na MTANZANIA walisema kuna hatari ya kupanda kwa bei za bidhaa kwa kile walichodai kuwa mifuko mbadala inauzwa bei ghali.

Uchunguzi wa MTANZANIA ulibaini mifuko mbadala inauzwa kati ya Sh 500 hadi 2,500 kutegemeana na ukubwa wa mfuko husika.

Juma Hassan ambaye ni mfanyabiashara ya miwa katika eneo la Karume, alisema hadi sasa bado hajajua atawawekea wapi wateja wake bidhaa hiyo.

“Miwa huwa nauza kuanzia Sh 200, 500 hadi 1,000. Sijajua kuanzia hiyo tarehe 1 wateja wangu nitawawekea wapi. Kuna hatari miwa tunayouza Sh 500 tukauza Sh 700 kutokana na gharama za mifuko mbadala,” alisema.

ILALA WATENGA MAENEO 36

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, alisema wametenga maeneo 36 katika ngazi ya kata kupokea mifuko ya plastiki na vituo 15 vya makampuni ya taka.

Alisema tangu Mei 9 walianza rasmi kutekeleza katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki na kwamba kuanzia Mei 29 walizindua maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo yataenda sambamba na uhamasishaji juu ya utumiaji wa mifuko mbadala.

Habari hii imeandaliwa na NORA DAMIAN (Dar), BENJAMIN MASESE (Mwanza) na ELIYA MBONEA (Arusha)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles