Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kwa kushirikiana na Serikali, UNFPA na Chama cha Wakunga Canada, wameandaa mafunzo maalumu ya huduma za dharura kwa wakunga ili kuimarisha uwezo wao wa kuhudumia akina mama wakati wa kujifungua na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Mafunzo hayo yanafanyika chini ya Mradi wa Thamini Uzazi Salama, ambao unalenga kuwajengea wakunga uwezo wa kushughulikia dharura wanapokuwa kwenye vituo vya afya.
Akizungumza leo Februari 10, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua mafunzo hayo ya siku tano, Rais wa TAMA, Dk. Beatrice Mwilike, amesema kuwa kundi la kwanza la wakunga 30 litapatiwa mafunzo, huku kundi lingine likitarajiwa kupatiwa mafunzo siku 10 zijazo, hivyo kufanikisha jumla ya wakunga 90 kupatiwa mafunzo hayo.
“Mafunzo haya yatawajengea wakunga uelewa wa jinsi ya kusaidia akina mama wanaopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua, kukabiliana na vikwazo vya uzazi, na kutoa msaada wa dharura kwa mama anayeshindwa kujifungua kawaida,” alisema Dk. Mwilike.
Kwa upande wake, Agness Mgaya, Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto Dar es Salaam, amesema mafunzo hayo yatasaidia wakunga kupata maarifa mapya kwani huduma za afya ni sayansi inayobadilika kila siku.
Alisema pia kuna changamoto kubwa ya ushiriki wa wanaume katika huduma za afya ya uzazi, kwani ni asilimia 47 pekee ya wanaume wanaoshiriki kuwahudumia wake zao wakati wa ujauzito na kujifungua. Alitoa wito kwa wanaume kuwasindikiza wake zao kliniki na hospitalini ili kuwapa faraja na kupunguza msongo wa mawazo.
Wakunga walioshiriki mafunzo hayo, Paul Zakaria na Sarah Hallan, wamesema maarifa waliyopata yatawasaidia kuboresha huduma na kuwasaidia wenzao kwenye vituo vya afya.
Mradi huu wa miaka saba unatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga, kutokana na viwango vya juu vya vifo vya akina mama na watoto katika mikoa hiyo.