Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Taasisi ya Utafiti ya Mifugo Tanzania (TALIRI) imeanzisha Teknolojia mpya kwa ajili ya ufugaji mifugo bila ya kutumia dawa ya aina yoyote ambayo haina kemikali.
AkizungumzaJulai 7, 2023 jijini Dar es Salaam katika maonyesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara sabasaba Mtafiti wa Kanda ya Afrika Mashariki, Paluku Emmanuel amesema Teknolojia hiyo ni ufumbuzi kutoka nchini Indonesia ambayo imepitia chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa miaka miwili na imeonyesha ufanisi mzuri katika ufugaji.
“Ni Teknolojia kutoka nchini Indonesia ambayo hakuna haja ya kutumia dawa ya aina yoyote, lengo kubwa ni kufuga kwa njia ya asilia na inayohakikisha mfugo husika unakuwa bila ya kutumia kemikali,”amesema Emmanuel.
Amesema Teknolojia hiyo inahimiza ufugaji asilia usiotumia dawa aina yoyote na Mifugo kukua kwa kiwango kinachoridhisha na katika ufugaji wa kuku, ng’ombe, nguruwe na mifugo mingine.
Amesema wizara hiyo imeshaifanyia utafiti dawa hiyo imeonekana haina tatizo lolote kwa mifugo.
“Tumejaribu kutumia dawa hiyo kwa kuku 400 waliotumia dawa hiyo asilimia Tano walikufa na wasiotumia asilimia 17 walikufa hapo utaona ni jinsi gani dawa hiyo ilivyokuwa na umuhimu kwa mifugo,” amesema.
Emmanuel amesema kuku waliotumia dawa hiyo wamekuwa na kilo 2.3 na wasiotumia wanakilo 2.1 kwa muda wa miezi mitatu.
Aidha, amesema dawa hiyo pia inaponyesha mifugo ugonjwa wa miguu na midomo.
Ameongeza kuwa dawa hiyo ina manufaa kwa mifugo na pia inaunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika usafirishaji wa nyama iliyobora na yenyewe viwango vya ali ya juu.
Naye, mmoja wa wateja katika banda Hilo ambae ni mfugaji Getruda Wakili ameisema yeye anapendelea kutumia Teknolojia za TALIRI kwa kuwa Zina ubora wa hali juu katika mifugo.
“Mimi binafsi nitaendelea kutumia Teknolojia hizi kwa sababu naona zinamanufaa kwa mifugo yangu,” amesema Getruda.