Na Ramadhan Hassan,Dodoma
Taasisi ya Taifa ya Mifugo (Taliri Mpwapwa) imesema kutokana na upungufu wa ubora wa malisho, upo umuhimu wa kuotesha aina bora za malisho kwa kuzingatia utayarishaji wa shamba, kurutubisha ardhi na upandaji.
Hayo yameelezwa Mtafiti wa Malisho kutoka Taasisi hiyo, Dk. Malongo Mwalingo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari,wakati ya ziara iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
COSTECH ilifanya mafunzo pamoja na ziara ya kuwatembelea watafiti na Taasisi za utafiti kwa waandishi wa habari za Sayansi katika mikoa ya Dodoma na Singida.
Mtaalamu huyo amesema kutokana na upungufu wa ubora wa malisho, upo umuhimu wa kuotesha aina bora za malisho kwa kuzingatia utayarishaji wa shamba, kurutubisha ardhi na upandaji.
“Katika utayarishaji wa shamba endapo shamba lako lina miti au vichaka inabidi kwanza lisafishwe ili kurahisisha ulimaji, shamba linaweza kusafishwa kwa kutumia moto, kufyeka na kung’oa au njia zote tatu kwa pamoja na baada ya kusafisha, kazi ni kulima na upandaji.
“Mkulima anapaswa kuhakikisha amepiga ‘harrow’ ili kulainisha udongo kurahisisha uotaji wa mbegu za malisho ambazo nyingi huwa na umbo dogo,kurutubisha ardhi ni muhimu ili kurekebisha upungufu wa madini mbalimbali yanayohitajika na mimea,”amesema.
Pia anasema katika kufanya hivyo unaweza kutumia Samadi, mboji au mbolea za chumvi chumvi ambapo upandaji wa mbegu za malisho unafaa kuzingatia ubora wa mbegu, wakati wa kupanda, na njia za kupanda.
Hata hivyo Mwalongo anasema ubora wa mbegu unapaswa kuzingatiwa kutokana na sehemu zinazoaminika kama vile Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Mabuki, vituo vya Utafiti wa Malisho ya Mifugo kama Kongwa na Mpwapwa (Dodoma).