TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
TANZANIA imeungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Haki ya Mtoto pamoja a kusherehekea miaka 30 ya utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa haki ya mtoto.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alisema kuwa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto ulipitishwa rasmi na nchi wanachama wa umoja huo Novemba 20, 1989 sambamba na uanzishwaji wa mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto ambapo hadi sasa nchi 190 zimetia saini na kuridhia.
“Hata hivyo kuna idadi kubwa ya watoto duniani wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukiukwaji mkubwa wa haki za mtoto na ukatili wa aina mbalimbali kama vipigo, kubakwa, mimba na ndoa za utotoni, ukeketaji, ulawiti, vitisho, umasikini unaowanyima mahitaji ya msingi, utumikishwaji, kuhusishwa na vita vinavyopelekea ulemavu na hata kupoteza maisha,” alisema Dk. Ndugulile.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa hali ya afya na watu na viashiria vya malaria (TDHS-MIS 2015/2016) zinaonyesha kuwa wasichana balehe wanne kati ya 10 wamefanyiwa ukatili wa kimwili na asilimia 17 wamefanyiwa ukatili wa kingono kati ya umri wa miaka 15-19.
Aidha, Dk. Ndugulile alisema mtoto mmoja kati ya wawili wa kike na kiume wa umri wa miaka 13-19 wamefanyiwa ukatili wa kimwili na pia mtoto mmoja kati ya 10 wa kike amefanyiwa ukatili wa kingono na mwalimu wake.
“Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 27 ya wasichana wenye umri wa miaka 15-19 wamezaa; na asilimia 57 ya wanawake wa umri wa miaka 19 wameshakuwa na watoto ambapo wasichana wawili kati ya watano wameolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.
“Aidha, kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi nchini za mwaka 2017, zinaonyesha kuwa matukio 13,457 ya ukatili dhidi ya watoto yaliripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi nchini ukilinganisha na matukio 10,551 kwa mwaka 2016.
“Taarifa hiyo inaonyesha kuwa mikoa mitano ya kipolisi inayoongoza kwa kuwa na takwimu kubwa za ukatili ni Kinondoni (2,426), Dodoma (1,283), Tanga (1,064), Temeke (984) na Arusha (972),” alisema Dk. Ndugulile.
Alisema katika maadhimisho ya mwaka huu, wizara imeshirikiana na wadau ambapo kwa kutafakari upatikanaji wa haki za mtoto, ambazo zimeainishwa vizuri na sera yetu ya mtoto ya 2008; haki hizo ni haki ya kuishi, kuendelezwa, kulindwa, kushiriki, kushirikishwa na kutobaguliwa.
Kwa upande wake, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, alisema wakati Tanzania inasaini mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kulinda haki za watoto mwaka 1991, yeye alikuwa rais na amefurahi kuona alichotarajia sasa watoto wanaweza kuzungumzia changamoto zao.
“Yote yanayosemwa na watoto yazingatiwe na changamoto zao zitatatuliwe, ikiwamo kuwalinda na kuwaepusha na ukatili mbalimbali.
“Kama wazazi tujenge ukaribu kwa watoto na kufuatilia makuzi yao hasa wanapokuwa nyumbani, shuleni na hata sehemu zingine,” alisema
Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (Unicef), Rene Van Dongen, alisema kuwa jamii inatakiwa kuwahusisha watoto na vijana katika hatua zote za upangaji, usimamizi, utekelezaji na tathmini wakati wa kutunga sera ili kuyachukua maoni yao kwa umakini.