Na Sheila Katikula, Mwanza
MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mwanza, Frank Mkilanya, amewataka wakuu wa taasisi mkoani hapa kuhakikisha wanawasilisha taarifa zao za mapokezi ya fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo mapema iwezekanavyo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Novemba 3,2021, Mkilanya amesema ni vema kuwasilisha taarifa hizo mapema ili kuongeza uwazi kwani kila mwananchi.
“Mkibaini kuna utekelezaji mbovu wa miradi ni vema mtoe taarifa TAKUKURU, kwani kila mtu anajukumu la kulinda fedha hizi ili miradi ikamilike mapema, kwa maana vitendo vya rushwa katika miradi vinarudisha maendeleo nyuma,” amesema.
Amesema TAKUKURU kupitia mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu ilitembelea miradi 74, kati ya hiyo miradi minne ilikataliwa na kiongozi wa mbio za mwenge.
“Miradi iliyokataliwa ni mradi wa maji wa kata ya Ng’haya wa Wilaya ya Magu, mradi wa mzani wa mazao ya samaki mwaloni uliopo Wilaya ya Ilemela, mradi wa bodaboda stendi ya mabasi Nansio Ukerewe na mradi wa maji Tabaluka Nyampande uliopo wilayani Sengerema.
Amesema changamoto zilizofanya miradi hiyo kukataliwa ni gharama za ujenzi kuwa kubwa ukilinganisha na uhalisia, kutokuwepo kwa nyaraka muhimu kama barua ya mapokezi ya fedha na maelekezo ya matumizi ya fedha na vifaa duni vya ujenzi.
“Kutokana na sababu hizo TAKUKURU imefungua majalada ya uchunguzi na tupo katika hatua mbalimbali, pindi itakapobainika kuna ubadhirifu wa fedha unafanyika wahusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,”amesema Makilya.