28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Takukuru yataja mikoa vinara kutafuna fedha za ushirika

NORA DAMIAN

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetaja mikoa mitano yenye kiwango kikubwa cha fedha zinazoendelea kuchunguzwa kutokana na ubadhirifu katika vyama vya ushirika nchini.

Fedha hizo Sh bilioni 31.7 ni sehemu ya Sh bilioni 124 zilizobainishwa katika ripoti ya ukaguzi wa vyama vya ushirika ya mwaka 2018/19 ambayo Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga aliikabidhi Takukuru ili ichunguze ubadhirifu huo.

Akizungumza jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, alisema walikabidhiwa ripoti hiyo Novemba 26 mwaka jana na hadi sasa wameshafanya uchunguzi kwa awamu mbili.  

“Uchunguzi wetu pia umebaini kwamba mikoa mitano ndiyo yenye kiwango kikubwa cha fedha zinazochunguzwa, tunaendelea kutoa wito kwa viongozi wa vyama vya ushirika na wafanyabiashara walionunua mazao ya wakulima au mtu mwingine yeyote mwenye fedha za ushirika arejeshe mara moja,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

Aliitaja mikoa hiyo na kiasi cha fedha kwenye mabano kuwa ni Njombe (Sh bilioni 7.9), Kagera (Sh bilioni 7.5), Kinondoni (Sh bilioni 5.9), Temeke (Sh bilioni 5.7) na Mbeya (Sh bilioni 4.7).

Alisema katika awamu mbili za uchunguzi wameokoa Sh bilioni 8.8 kati Sh bilioni 66.2 zilizochunguzwa.

Alifafanua kuwa katika awamu ya kwanza uchunguzi ulihusisha Sh bilioni 51.7 na kati ya hizo Sh bilioni 4.066 ziliokolewa na kwamba awamu ya pili ilihusisha uchunguzi wa Sh bilioni 14.4 na kati ya hizo zimeokolewa Sh bilioni 4.8.

Alisema baadhi ya fedha hizo zimerejeshwa kwa wakulima na vyama vya ushirika na zingine kutunzwa katika akaunti maalumu, huku akisema kuwa katika awamu inayofuata hawatakuwa na huruma na mtu yeyote aliyefisadi fedha za vyama vya ushirika.

Brigedia Jenerali Mbungo alisema awamu ya tatu itahusisha uchunguzi wa Sh bilioni 57.3 katika vyama mbalimbali vilivyopo katika mikoa 27 nchini.

Mikoa hiyo na kiwango cha fedha kitakachochunguzwa kwenye mabano ni Ruvuma (Sh bilioni 1.6), Kilimanjaro (Sh milioni 153.9), Manyara (Sh milioni 78.4), Kinondoni (Sh bilioni 5.9), Katavi (Sh milioni 200.1), Pwani (Sh milioni 797.3), Mbeya (Sh bilioni 4.5), Iringa (Sh bilioni 3.9), Simiyu (Sh bilioni 1.2), Ilala (Sh bilioni 3.5) na Arusha (Sh bilioni 1.1).

Mingine ni Kigoma (Sh milioni 78.9), Lindi (Sh milioni 649.9), Njombe (Sh bilioni 4.054), Tanga (Sh milioni 322.1), Tabora (Sh milioni 420.4), Shinyanga (Sh bilioni 1.5), Mara (Sh bilioni 2.3), Temeke (Sh bilioni 5.4), Mwanza (Sh bilioni 3.9), Kagera (Sh bilioni 7.2), Geita (Sh milioni 21.2), Songwe (Sh milioni 685.2), Rukwa (Sh milioni 596.6), Morogoro (Sh bilioni 1.7), Dodoma (Sh bilioni 3.5) na Mtwara (Sh bilioni 1.2).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles