Amina Omari,Tanga
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Tanga imefanikiwa kuokoa kiasi cha Sh milioni 18.4 zilizokuwa kwa ajili ya malipo hewa pamoja na ukwepaji wa Kodi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Christopher Mariba wakati akitoa taarifa ya utendajikazi wa taasisi hiyo kwa kipindi Cha Mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka jana.
Alisema kuwa kati ya fedha hizo Sh milioni 16 ziliokolewa kutokana na malipo hewa, huku Sh milioni mbili ikiwa ni ukwepaji wa Kodi.
Aidha, kuu huyo alisema kuwa wameweza kubaini kasoro mbalimbali katika miradi ya maendeleo waliyoweza kuipitia na kuifanyia tathimini.
“Tumeweza kufanya ufuatiliaji miradi 17 ya maendeleo iliyoko katika sekta mbalimbali mkoani hapa na kubaini mapungufu kadhaa ikiwemo usimamizi duni, kutokuwepo na ufuatiliaji pamoja na uhujumu,” alisema Mariba.
Alisema kuwa Serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi katika miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.
“Kumekuwa na changamoto kwa watumishi wasio na uadilifu katika usimamizi wa miradi hivyo sisi kama taasisi ni jukumu letu kuhakikisha tunadhibiti mianya yote ya Rushwa ili miradi hiyoiweze kukamilika kwa wakati,” alisema.
Vile vile alisema kuwa katika kipindi hicho taasisi imeweza kupokea jumla ya taarifa za rushwa zipatazo 129, huku taarifa 76 uchunguzi wake ukiwa unaendelea na wakifungua mashauri kesi 20.