SHOMARI BINDA -MUSOMA
MWALIMU mstaafu, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, ameishukuru Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mara kumsaidia kuokoa fedha zake zaidi ya Sh milioni 14.
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu kilichomkuta baada ya kuchukua mkopo kwa wakopeshaji wa mtaani, alisema kama si kusaidiwa na taasisi hiyo, nyumba yake ingeuzwa kutokana na mkopo aliochukua.
Mwalimu huyo alisema alichukua mkopo wa Sh milioni 7,200,000 na akatakiwa kurejesha Sh milioni 24 na riba ilikuwa Sh milioni 16.8.
Alisema baada ya kusikia taarifa ya Takukuru ya kuwafuatilia wakopeshaji wasio waaminifu na kuwataka waliokopeshwa kwenda kutoa taarifa aliamua kwenda ili asikilizwe.
Mstaafu huyo alisema baada ya kusikilizwa, maofisa wa Takukuru waliingilia kati suala lake na kufanikiwa kumsaidia kuokoa zaidi ya Sh milioni 14.
“Naishukuru taasisi hii kwa msaada mkubwa walionipatia katika suala langu lililokuwa likinikabili.
“Nilikopa kidogo, riba ilikuwa kubwa, nikatakiwa kurejesha kiasi kikubwa cha fedha, bila msaada niliopata ningeweza hata kuuziwa mji wangu na mimi ni mstaafu na nina familia kubwa,” alisema.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Alex Kuhanda, alisema baada ya kufuatilia jambo hilo, mwalimu huyo alirejesha Sh 9,744,000 na riba ambayo ilikuwa Sh 2,544,000, badala ya Sh milioni 16,800,000 na hivyo kuokoa Sh milioni 14.2.
Kuhanda aliwataka wastaafu au hata watumishi walio katika utumishi kuacha kukopeshwa kwa riba zisizokubalika na wale walioingia kwenye ukopeshaji usiofaa kufika kwenye ofisi za Takukuru na kutoa taarifa.