30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Takukuru wajitosa rasmi rushwa ya ngono UDSM

 Waandishi wetu Dar/Kilimanjaro

IKIWA ni takribani siku 10 tangu Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Vicensia Shule, kutoa tuhuma za rushwa za ngono chuoni hapo kupitia akaunti yake ya mtandao wa twitter, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imesema tayari imeanza uchunguzi wa suala hilo.

Katika akaunti yake ya Twitter, Dk. Shule alindika;  “Baba @MagufuliJP (Rais John Magufuli) umeingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufungua maktaba ya kisasa. Rushwa ya ngono imekithiri mno UDSM. Nilitamani nikupokee kwa bango langu ila ulinzi wako umenifanya ninyamae. Nasubiri kusikia toka kwako maana naamini wateule wako ni waadilifu watakwambia ukweli.”

Taarifa hiyo ya Dk Shule ilionekana kutikisa kwenye mitandao ya kijamii na chuoni hapo, ambapo Kamati yake ya Maadili ilikutana na msomi huyo.

Baadaye Mwenyekiti wa kamti hiyo, Profesa Eveline Mbede, alisema kamati yake imemaliza kazi na haitaendelea kufuatilia tuhuma za kashfa ya ngono katika chuo hicho kwa kuwa tayari zimepelekwa Takukuru.

“Kwa kuwa alitueleza kuwa ameshafikisha taarifa hizo Takukuru, taasisi ambayo ina mamlaka kamili na inayoaminika, sisi pia tuliona kwamba ni chaguo sahihi kwa kuwa alikuwa na uhuru. Ni aidha angetumia mfumo uliopo ndani ya chuo au kupeleka suala hilo Takukuru. Kwa kuwa aliamua kulipeleka Takukuru, tuliona pia ni sehemu sahihi na sisi tutakuwa tayari kutoa ushirikiano itakapohitajika,” alisema.

Kauli ya Takukuru

Jana Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani aliiambia Mtanzania kuwa suala hilo limeshapokelewa na ofisi yake na tayari linashughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu baada ya kupoeka maelezo ya awali kutoka kwa Dk. Shule.

Alisema kwa sasa tayari wameshaanza kufuatilia watuhumiwa na walalamikaji katika suala hilo na kwa sasa hawezi kuzungumzia kwa undani zaidi kwa kuwa suala hilo liko katika hatua za awali za upelelezi.

“Ni kweli, suala hilo limefikishwa kwetu na tunalishughulikia, kwa sasa siwezi kuzungumza kwa kuwa inaweza kuingilia upelekezi ambao uko katika hatua za awali,” alisema.

Alisema Takukuru itatoa taarifa kuhusu mwenendo wa suala hilo pale itakapoona inafaa na imefikia katika hatua ambayo kutakuwa na uwezekano wa kutoa taarifa ambazo hazitaingilia au kuvuruga upelelezi wao.

Dr shule afunguka tena

Kwa upande wake Dk Shule jana alisema tangu kutoa taarifa hizo, kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaomfuata kutoa taarifa juu ya kuombwa rushwa ya ngono.

“Wapo mpaka waliomaliza chuo, wamejitokeza na wapo tayari kutoa ushahidi,” alisema.

Alipouliuzwa kuhusu idadi, alisema suala hilo siyo muhimu kwasababu hata kama ni watu wawili wamejitokeza, inadhihirishwa kuwa kuna tatizo na suala la msingi ni kutokomeza tatizo bila kujali wingi wa waathirika.

“Rushwa ya kawaida tu huwezi kusema idadi ya waomba rushwa, sembuse hii ambayo ni ya usiri zaidi, suala la msingi hapa tutokomeze kabisa rushwa hii ya ngono,”alisema.

Kuhusu kuhojiwa na kamati ya maadili ya chuo, Dk Shule alisema kwa kiasi kikubwa walijadiliana kuhusu ukubwa wa tatizo hilo.

Makamu Mkuu wa Chuo

Baada ya taarifa ya Dk. Shule kutolewa kwa mara ya kwanza, Makamu Mkuu wa UDSM,  Profesa William Anangisye, alisema licha ya Dk. Shule kuandika tuhuma hizo kwenye mitandao ya kijamii, hayawahi kuzifikisha ofisini kwake.

Alisema inawezekana UDSM kuna matatizo mengi lakini tangu apewe jukumu la kukiongoza chuo hicho, hajawahi kufikishiwa tuhuma za rushwa za ngono.

Kwa mumkutadha huo alimtaka mwandishi arudi kumuuliza Dk. Shule maswali manne ambayo yeye alihoji.

Maswali hayo ni moja,  kwa nini hajawahi kuwasilisha tuhuma hizo ofsini kwa Makamu Mkuu wa Chuo?

Pili, kama Dk. Shule amewahi kufikisha taarifa hiyo kwenye menejimenti, afafanue ni menejimenti ipi, ya idara, college au chuo?

Tatu, Dk. Shule ni kiongozi ndani Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDASA) je suala hilo amewahi kulifikisha kwenye vikao vya jumuiya hiyo?

Nne,  kama tatizo hilo ni la muda mrefu kwa nini asubiri ujio wa Rais Dk. Magufuli  ndio aliwasilishe kwa njia ya mitandao ya kijamii?

Baada ya maswali hayo kwa Dk. Shule, Profesa Anangisye alisema yeye ana shahada ya uzamivu katika masuala ya uadilifu wa walimu hivyo anaamini kuwa ni wajibu wa mwalimu kulinda mwanafunzi.

“Na mimi nikimshika mtu nikapata ushahidi, taratibu za ualimu haziruhusu mtu wa aina hii kuendelea kuwa mwalimu na sio taratibu tu hata taratibu pia za nchi. Kwa hiyo pale atakapoonekana kwamba ni mwalimu hatutafumbia macho,” alisema Profesa Anangisye.

Majibu ya Dk. Shule

Mwandishi alirudi tena kwa Dk Shule kama alivyoelekezwa Profesa  Anangisye, ambapo  Dk. Shule alijibu kwa ujumla akimtaka kiongozi huyo wa chuo awaulize wasaidizi wake( Depute Vice Chancellor-DVC)

“Awaulize wasaidizi wake ni mara ngapi nimekutana nao kuwaelezea suala hili,” alisema Dk. Shule.

Dk Shule akizungumzia nafasi yake ya uongozi wa  UDASA na hatua alizochukua kuliwasilisha suala hilo ndani  jumuiya hiyo, alisema mara nyingi uongozi wa jumuiya hiyo umeshindwa kukutana kufanya vikao kwa sababu ya Makamu Mkuu wa Chuo kuwazuia kuitisha mikutano na kuwanyima ukumbi wa kufanyia mikutano.

Akijibu swali la kwanini amesubiri ujio wa Rais Dk. Magufuli ndio akaripoti tuhuma hizo kwenye mitandao ya kijamii, Dk. Shule alisema kwamba anahaki ya msiki ya kikatiba kufanya hivyo kama mwananchi.

Alisema yeye kuwa mtumishi wa umma sio sababu ya kuangusha haki yake ya kikatiba ya uhuru wa kujieleza.

Makamu wa Chuo tena

Baada ya maelezo ya Dk. Shule, gazeti hili lilirudi kwa mara nyingine kwa Profesa Anangis na kumueleza alichosema Dk Shule.

Profesa Anangisye aliendelea kuhoji kama Dk. Shule aliripoti taarifa hizo kwenye menejimeni na kwamba wasaidizi wake (DVC) wanajua na kama aliona mambo hayaendi kwa nini asingefika ofisini kwake kumtaarifu?

Alisema UDASA ina kamati ya utendaji kwa nini hajawahi kutoa taarifa hizo?

“Waliomba ukumbi na tulipozuia  hapajawahi kuwa na kikao chenye agenda ya suala la ngono. Angenda zote za UDASA hupitishwa na kamati tendaji na yeye ni mjumbe sijawahi kuona hoja kama hiyo anayotuhumu,” alisema Profesa Anangisye.

Alisema UDSM inawalimu zaidi ya 1200  inawezekana watuhumiwa ni watu 10 au 20 hivyo kusitumike madai hayo kuchafua wali wote.

Alisema Dk. Shule anatakiwa atoe takwimu za kutosha za wanafunzi walioathiriwa pamoja na ushahidi.

Baada ya mazungumzo hayo,  Profesa Anangisye alimpigia tena simu mwandishi na kumwambia kwamba anamsifu Dk. Shule kwa ujasiri aliouchukua.

“Hii ni alamu ya kuniamsha pia, kweli suala hili linafanyiwa kazi lakini alichokifanya kinaonyesha kuwa angalau kuna watu majasiri, amediriki kusema ukweli kama upo na kama haupo waja.

“Kwangu mimi namshukuru Mungu kwamba angalau nimempata mtu ambaye atanisaidia kupata data. Sema tu kama nilivyosema mwanzoni hajawahi kuja ofsini kwangu kunieleza jambo kama hili,” Profesa Anangisye.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles