Amina Omari, Tanga
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Tanga imefanikiwa kuokoa kiasi cha Sh milioni 63.7 zilizotokana na mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri, makusanyo ya mapato pamoja na kurejesha fedha zilizokopwa katika vya ushirika.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana Kamanda wa Taasisi hiyo mkoani hapa, Dk. Sharifa Bundala juu ya utendaji kazi wa TAKUKURU mkoani hapa kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka jana.
Amesema TAKUKURU wameweza kufanikiwa urejeshwaji wa Sh milioni 19.2 za Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, fedha ambazo zilitokana na makusanyo ya mapato na fedha hizo kushindwa kuingizwa kwenye akaunti ya Halmashauri.
“TAKUKURU baada ya kupata taarifa hiyo tulianza kufanya ufuatiliaji ikiwemo kuwahoji watumishi tisa ambao walikabidhiwa mashine za ukusanyaji mapato (POS) kwa ajili ya kukusanya mapato na kushindwa kuziwasilisha fedha hizo benki, hivyo kuhesabika kuwa ni deni katika akaunti zao,” amesema Kamanda huyo.