26.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

TAKUKURU Pwani yaanza ufuatiliaji wa vitendo vya rushwa kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Na Gustaphu Haule, Mtanzania Digital

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imeanza kufanya ufuatiliaji wa vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, Ally Sadick, alitoa taarifa hiyo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi zake mjini Kibaha, akielezea utekelezaji wa kazi za TAKUKURU katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2024.

Sadick alieleza kuwa TAKUKURU itafuatilia kwa ukaribu mwenendo wa wagombea wa uchaguzi huo, na kuchukua hatua stahiki pindi watakapobaini viashiria vya rushwa. Aidha, aliongeza kuwa taasisi hiyo itaendelea kutoa elimu juu ya madhara ya rushwa kwa wadau wote, wakiwemo vyama vya siasa, wasimamizi wa uchaguzi, wanahabari, wananchi, na jamii kwa ujumla.

“Tumejipanga kuendelea kutoa elimu kwa umma kwa wananchi, wanasiasa, viongozi wa dini, waandishi wa habari na wadau wote wanaoshiriki kwenye uchaguzi ili kuhakikisha tunakuwa na uchaguzi usio na vitendo vya rushwa,” alisema Sadick.

Sadick aliwahimiza wananchi wa Mkoa wa Pwani kuunga mkono jitihada za kupambana na rushwa kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kuwachukulia hatua wale wanaojihusisha na vitendo hivyo, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

Kwa upande mwingine, TAKUKURU Mkoa wa Pwani imesaidia kuokoa zaidi ya Sh bilioni 1.6 katika Halmashauri ya Mji Kibaha kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato katika kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu. Fedha hizo zilikusanywa baada ya kubaini uvunjifu wa sheria na taratibu za ukusanyaji wa mapato na baadhi ya watumishi kushindwa kuwajibika ipasavyo.

Sadick alifafanua kuwa ufuatiliaji uliofanywa na TAKUKURU ulibaini baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo kujihusisha na makubaliano yasiyo halali na wafanyabiashara, ikiwemo kuruhusu ulipaji wa ushuru mdogo usioendana na mauzo halisi, pamoja na kumiliki mashine za EFD zaidi ya moja ili kukwepa malipo sahihi.

Kuhusu uchunguzi na mashtaka, Sadick alisema TAKUKURU Mkoa wa Pwani ilipokea jumla ya malalamiko 95 katika kipindi hicho, ambapo 55 kati ya hayo yalihusisha vitendo vya rushwa. Aidha, alibainisha kuwa kesi mpya 11 zilifunguliwa mahakamani, na kati ya hizo, watuhumiwa saba walipatikana na hatia.

Sadick alisisitiza kuwa TAKUKURU itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wa vitendo vya rushwa na kuendelea kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa unafanyika bila vitendo vya rushwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles