27.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Takukuru kuboresha ufuatiliaji wa kesi za rushwa

Ashura Kazinja -Morogoro

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema iko mbioni kuboresha utaratibu wa kufuatilia kesi zinazohusu watuhumiwa wanaojihusisha na rushwa, ili kesi hizo zisichukue muda mrefu kama ilivyo sasa.

Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro baada ya kufika mkoani humo kwa ziara ya kikazi.

Jenerali Mbungo alisema hayo kufuatia taarifa fupi iliyotolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Kalobelo, iliyotaja changamoto katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na uwepo wa ucheleweshwaji wa kesi za watuhumiwa wanaojihusisha na rushwa kuchukua muda mrefu kufikishwa mahakamani.

Jenerali Mbungo alibainisha kuwa, kiongozi wa kwanza hapa nchini kutamka changamoto ya watuhumiwa wa rushwa kuchelewa kuchukulia hatua ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.

“Kwanza aliyeliona kwamba linachelewa ni Rais na akatuagiza tubadilishe utaratibu, kwa hiyo niwape matumaini kuwa ucheleweshaji huu katika kushughulikia kesi za watuhumiwa wa rushwa utamalizwa ndani ya mkoa.

 “Kwa hiyo, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) mkoani ndiye atashughulikia tuhuma zote ambazo zitapaswa kubaki mkoani. Kwa hiyo, adha ile ya kuona watuhumiwa wanarandaranda barabarani huku wakiwa wanatuhumiwa itakuwa imepungua kama sio kuisha kabisa,” ” alisema Jenerali Mbungo.                                                                                                            

Alisema kwa bahati nzuri kama ofisi wameshafanya mapitio ya sheria zinazohusika na tuhuma zote zitakazokuwa zinajitokeza ndani ya mkoa na kupaswa kubaki mkoani zitakuwa zinamalizwa ndani ya mkoa, na hivi karibuni sheria hiyo itaanza kutumika kikamilifu.

Aliongeza kuwa awali utaratibu ulikuwa kesi hizo zilikuwa zinaanzia ngazi ya wilaya, kwenda mkoani, Makao Makuu ya Taasisi hiyo na baadae kwenda kwa  DDP hali ambayo ilikuwa inachangia kuchelewesha kukamilika kwa kesi hizo zinazohusu rushwa hapa nchini.

Pamoja na kueleza hayo, Mkurugenzi huyo wa Takukuru alishukuru ushirikiano uliopo wanaoupata kutoka ofisi za wakuu wa mikoa kwa watendaji wake wa Takukueu ngazi ya mkoa na kusema mafanikio yote yanayopatikana kwa sasa ni kutokana na uwepo wa ushirikiano mzuri baina ya pande hizo mbili.

Awali, akiwasilisha taarifa fupi mbele ya Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Katibu Tawala  Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Kalobelo, alisema kuna wakati inaonekana wazi kuwepo kosa la wazi kwa mtuhumiwa, lakini itachukua muda mrefu mtuhumiwa huyo kufunguliwa mashtaka kutoakana na mlolongo mrefu uliopo unao sababishwa na taratibu zilizopo na kuomba kuangalia kwa mapana utaratibu huo.

Changamoto nyingine ambayo iliwasilishwa na Katibu Tawala huyo ni kuomba kuwepo Ofisi ya Takukuru Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ambapo alisema Halmashauri hiyo bado ina changamoto nyingi na iko umbali wa zaidi ya kilometa 100 kutoka Manispaa ya Morogoro hadi Mvuha yalipo Makao Makuu ya Halmashauri hiyo, hivyo ofisi hiyo inahitajika ili kurahisisha kazi zinazohusiana na Rushwa.

Brigedia Generali John Mbungo aliteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Agosti 21, 2017 na Machi 26 mwaka huu aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Takukuru hapa nchini kutokana na kazi nzuri anayoifanya.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,530FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles