Na Mohamed Hamad, Kiteto
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,(TAKUKURU) wilayani Kiteto Mkoani Manyara, imeokoa Sh milioni 6.6 mali ya, Bakari Lugage mstaafu alizokuwa ameporwa na moja ya taasisi ya fedha.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Manyara, Holle Makungu amesema Taasisi nyingi zinafanya kazi bila sheria na kanuni zinazoongoza utendaji wao wa kazi hali inayofanya wamiliki kujiamulia bila kujali madhara kwa wananchi.
Amesema serikali kupitia bunge kwa kuona udhaifu huo lilitunga sheria ya huduma ndogo ya fedha ya mwaka 2018 na kufuatiwa na kanuni zake zilizotangazwa kwenye gazeti la serikali Na. 679 la tarehe 13.09.2020.
Aidha, Makungu amesema udhaifu huo umefanya Lugage aliyekuwa amekopa Sh milioni 1.4 mwaka 2018 kwa moja ya kampuni Kiteto kulipa Sh milioni 8.
Amesema Takukuru ilibaini mzee huyo mwishoni mwa mwaka 2018 ambapo alianza kukopa fedha kati ya Sh 50,000 hadi 100,000 kwa nyakati tofauti huku dhamana yake ikiwa ni kadi ya Benki (ATM).
Baada ya kiinua mgogo chake kuingia kampuni hiyo ya kifedha iliyopo Kiteto ilichukua kiasi cha Sh milioni 8 kwenye akaunti yake na alipofuatilia kwa muda mrefu hakufanikiwa ndipo akafika kuomba msaada Takukuru.
Akimkabidhi fedha hizo Sh milioni 6.6, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Kanali Patrick Songea amewaasa wananchi kuwa makini na taasisi kifedha na kuwataka kusoma na kuielewa mikataba kabla ya kuisaini.
“Wananchi kuweni makini katika mikataba kwa makampuni haya kwani ni wengi wanalalamika na wakati mwingine ni kutoona umuhimu wa kuwa na mikataba jambo ambalo ni la msingi,” amesema Kanali Songea.
Kwa upande wake, Lugage baada ya kukabidhiwa fedha zake alishukuru Taasisi hiyo kuwa imekuwa msaada mkubwa kwani pamoja na kufuatilia kwa muda aligonga mwamba.
“Hata mipango yangu ilikufa sikuwa na la kufanya maana hela zangu zilishapotea ila sasa itabidi nijipange tena upya kuanzisha mipango yangu ya maendeleo,” amesema Lugage