25.5 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Takukuru kicheko

Nora Damian -Dar es Salaam

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imesema fedha zilizookolewa kutokana na udhibiti wa vitendo vya rushwa, zimeongezeka kutoka Sh blioni 70.3 (2017/18) hadi Sh bilioni 82.8 (2018/19).

Akizungumza jana wakati wa kuwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, alisema Sh bilioni 82.8 zimeokolewa kwenye operesheni mbalimbali ambazo zinahusisha fedha taslimu Sh bilioni 5.5, mali zenye thamani ya Sh bilioni 59.1 na Sh bilioni 18.2 zilizodhibitiwa.

Brigedia Jenerali Mbungo alisema mali zilizokolewa zinahusisha jengo la ghorofa moja na kituo cha mafuta vilivyotaifishwa jijini Mwanza vyenye thamani ya Sh bilioni 10.1 baada ya mmiliki wake kubainika kuzipata kwa njia ya rushwa, huku mali zenye thamani ya Sh bilioni 49 zikirejeshwa serikalini.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mali hizo ni zile za viwanda na mashirika yaliyobinafsishwa zikiwamo zenye thamani ya Sh bilioni 15 za kiwanda cha Mang’ula Morogoro, Sh bilioni 13.6 za Shirika la National Steel lililopo Temeke, Dar es Salaam, Sh bilioni 7.5 za Kiwanda cha Korosho Nachingwea, Sh bilioni 7 za Kiwanda cha Korosho cha Mtama na Sh bilioni 5.9 za Kiwanda cha Chai Mponde.

“Sh bilioni 25.3 zimewekewa zuio, Dola milioni 5.7, magari 14 na nyumba 16 kwa lengo la kukamilisha taratibu za kisheria za kutaifisha na kurejesha serikalini,” alisema.

HALI YA RUSHWA

Alisema tathmini ya hali ya rushwa hufanywa na taasisi za kimataifa na ndani ya nchi ikiwemo Taasisi ya Transparency International na Jukwaa la Uchumi Duniani.   

Taasisi ya Transparency International hupima hali ya rushwa kwa kutumia kiashiria kinachotumia mizani ya alama 0 hadi 100 wakati Jukwaa la Uchumi Duniani hupima ufanisi katika matumizi ya fedha za umma.

Kwa mujibu mkurugenzi huyo, utafiti wa mwaka 2019 wa Taasisi ya Transparency International unaonyesha Tanzania ilipata alama 37 na kushika nafasi ya 96 kati ya nchi 180, ikilinganishwa na alama 30 katika nafasi ya 119 ambayo ilipata kabla ya awamu ya tano kuingia madarakani.

“Katika nchi za maziwa makuu barani Afrika, Tanzania imeendelea kushika nafasi ya pili tangu mwaka 2015 hadi sasa.

“Pia mtazamo wa wananchi na uzoefu kuhusu rushwa katika kipengele cha juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa Tanzania imekuwa ya kwanza katika nchi 35 za Afrika zilizofanyiwa utafiti,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

Alisema pia Watanzania wenye imani kwamba Serikali inafanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa wameongezeka kutoka asilimia 37 (2015) hadi kufikia asilimia 71 (2019).

Aidha alisema idadi ya wanaoamini vitendo vya rushwa vimepungua imeongezeka kutoka asilimia 13 mwaka 2015 hadi asilimia 72 mwaka 2019.

Alisema pia ripoti ya 2019 ya Jukwaa la Uchumi Duniani kuhusu ufanisi katika matumizi ya fedha za umma imebainisha Tanzania imeshika nafasi ya 28 kati ya nchi 136 zilizofanywia utafiti.

Kuhusu miradi ya maendeleo iliyofuatiliwa, alisema imeongezeka kutoka 691 yenye thamani ya Sh bilioni 1,494 hadi 1,106 yenye thamani ya Sh bilioni 1,668.

Alisema miradi 113 yenye thamani ya Sh bilioni 99 kati ya 1,106 ilibainika kuwa na mapungufu ikiwemo ubadhirifu na taratibu za manunuzi.

“Tulifanya uchunguzi dhidi ya madai ya wakulima katika vyama vya ushirika ambapo Sh bilioni 8.8 zimeokolewa na kurejeshwa kwa wakulima waliodhulumiwa nchini.

“Pia tumefanikiwa kuokoa fedha za korosho zilizopotea Sh milioni 265 kati ya Sh milioni 570,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

UTENDAJI KAZI

Kuhusu utendaji kazi wa Takukuru kwa mwaka 2018/19, alisema majalada 911 ya tuhuma mbalimbali yalifunguliwa na kati ya hayo 266 yanahusu hongo na 645 vifungu vingine vya sheria.

Alisema majalada 388 yaliombewa kibali cha kufikisha watuhumiwa mahakamani na 277 yalipata kibali yakiwemo tisa ya kesi za rushwa kubwa.

Kulingana na mkurugenzi huyo, kesi mpya 497 zilifunguliwa na kufanya jumla ya kesi kufikia 1,013, zikiwamo kesi nne za rushwa kubwa katika Mahakama ya Mafisadi.

“Kesi 341 ziliamuliwa ambapo 206 watuhumiwa walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa faini na 135 hawakukutwa na hatia. Kiwango cha kushinda kesi kiliongezeka kufikia asilimia 62.41 ikilinganishwa na asilimia 60.1 ya 2017/18,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

Hata hivyo alisema wamebaini kuwapo kwa migongano ya kisheria katika ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa kielektroniki katika mradi wa mabasi yaendayo haraka na kuikosesha Serikali mapato.

Kasoro nyingine zilizobainika ni za uchache wa mashine za kukusanyia mapato na mianya ya rushwa katika ukusanyaji kodi ya majengo.

Aliishauri Mamlaka ya Mapato (TRA) kutafuta suluhisho kati yake na halmashauri katika ukusanyaji kodi za majengo.

Kasoro nyingine ni katika uandaaji na usimamizi wa mitihani ya taifa ambapo ilibainika wasimamizi kutoa na kupokea rushwa ili kufanya udanganyifu, wanafunzi kukamatwa na majibu na kufanyiwa mitihani na watu wengine.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles