Tunu Nassor -Dar es salaam
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ilala imesema imefungua mashauri 27 mahakamani yanayohusisha rushwa na ubadhirifu wa mali za umma yakiwamo mashauri mawili yanayowahusu wanasiasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akitoa ripoti ya miezi mitatu Oktoba hadi Desemba mwaka jana kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Takukuru Ilala, Christopher Myava alisema mashauri hayo yapo katika hatua mbalimbali za usikilizwaji.
Alisema mashauri mawili ya wanasiasa wa CCM yanahusisha rushwa ingawa hakutaka kuelezea kwa undani kwa kuwa yapo mahakamani.
Alisema yanayohusisha watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yapo matano, na yanayohusu watumishi wa Serikali za mitaa ni manne.
“Katika mashauri hayo kuna manne ya watumishi wa idara ya afya, elimu ya juu mawili, idara ya elimu mawili na vyama vya siasa mawili,” alisema Myava.
Alisema pia kuna mashauri mawili yanayohusisha wafanyabiashara, utapeli moja, baadhi ya watumishi wa taasisi za fedha moja, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira(Dawasa) moja na Idara ya Kilimo shauri moja.
Aliongeza kuwa wanawashikilia viongozi sita wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania(TALGWU Saccos) kwa ubadhirifu wa Sh bilioni 1.6.
Alisema viongozi hao wanashikiliwa baada ya kubainika kutoa fedha hizo kwa madai ya kuwakopesha wanachama hewa 91 na hivyo kusababisha upotevu wa fedha hizo
“Tunafanya uchunguzi wa vyama vyote vya ushirika kwani tumebaini baadhi ya viongozi wamekuwa wakijinufaisha kwa kufanya ubadhirifu,” alisema Myava.
Alisema pia wanawashikilia watu watatu waliokuwa wakijifanya watumishi wa umma na uchunguzi dhidi ya makosa yao utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa.
Myava pia alisema katika kuhakikisha wanabaini mianya ya rushwa na kupata njia sahihi ya kuishauri Serikali, wamefanya uchambuzi wa mfumo wa matumizi fedha za ruzuku ya uendeshaji.
“Tumefanya uchambuzi wa mfumo wa Uandikishaji wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kubaini kama kunaweza kuwapo kwa mianya ya rushwa na kutoa ushauri kwa Serikali,” alisema Myava.
Alisema katika kipindi hicho cha miezi mitatu wamefanya ukaguzi na ufuatiliaji wa miradi yenye thamani ya Sh bilioni 13.5 inayotekelezwa na Serikali ukiwamo wa ujenzi wa machinjio ya Vingunguti.