Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imekamata mbolea ya ruzuku iliyokuwa ikiuzwa kwa bei ya juu kinyume na utaratibu wa serikali.
Akizungumza Jumatano, Januari 29, 2025, Jijini Dodoma, Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo, Victor Swella, amesema mbolea hiyo ilikuwa ikiuzwa kwa Sh 150,000 badala ya bei elekezi ya Shilingi 75,000 kwa wakulima.
“Katika tukio hili, tulifanikiwa kumkamata mfanyabiashara mmoja na kumfungulia kesi namba 32320/2024 katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma. Mshtakiwa alishtakiwa kwa kuuza mbolea bila kibali, alikiri kosa na Mahakama ilimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela au faini ya Shilingi milioni 2,” amesema Swella.
Ameeleza kuwa mshtakiwa alilipa faini hiyo na kuachiwa huru.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU imefanikiwa kuokoa Shilingi milioni 66 zilizokuwa hazijapelekwa benki kutoka makusanyo ya POS mashine katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa.
“TAKUKURU Mkoa wa Dodoma imeweka utaratibu wa kufuatilia taarifa za makusanyo ya POS kila Jumatatu ili kubaini mapato ambayo hayajapelekwa benki kwa wakati. Kupitia ufuatiliaji huu, tumefanikisha kuokoa Sh milioni 66 zilizokuwa hatarini kupotea,” amesema Swella.
Amesisitiza kuwa taasisi hiyo itaendelea kufuatilia kwa karibu ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa manufaa ya wananchi.