TAIFA STARS YA COSAFA NA MALALAMIKO YA WATANZANIA

0
950

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

BENCHI la ufundi la kikosi cha timu ya soka Taifa Tanzania (Taifa Stars) limetua idadi ya wachezaji 22 wanaounda kikosi hicho kujiandaa na michuano ya Baraza la Mpira wa Miguu la nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA) ambako Taifa Stars imealikwa kushiriki michuano hiyo kama nchini mwalikwa na mwanachama wa Baraza la soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Michuano hiyo inayofanyika nchini Afrika Kusini, itakishuhudia kikosi cha Taifa Stars kikiwa sehemu ya timu zitakazoshiriki michuano hiyo inayotumika kuwatafutia fursa wachezaji wa nchi za Kusini mwa Afrika kuonekana na kusajiliwa.

Mara mwisho Tanzania kushiriki michuano hiyo ilikuwa mwaka 2015, ambako Taifa Stars ilienda nchini humo na kutolewa kwenye hatua ya makundi.

Baada ya timu kuonyesha kiwango cha chini katika fainali hizo kila Mtanzania alitaka aliyekuwa kocha wa kikosi hicho Mholanzi Mart Nooij kutimuliwa kazi, lakini viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) walikuwa wazito kufanya mabadiliko hayo ya benchi la ufundi na badala yake walikuja kufanya mabadiliko hayo baada ya Taifa Stars kufungwa mabao 3-0 dhidi ya Uganda (The Cranes) mchezo wa kutafuta nafasi ya kushiriki Mataifa Afrika nchini Rwanda.

Hivyo kila Mtanzania anapoikumbuka michuano hii ya COSAFA, kitu cha haraka kinachokuja ndani ya kumbukumbu zake ni uwepo wa Nooij katika benchi la ufundi la Taifa Stars na kiwango cha chini kwenye michuano hiyo.

Wakati huu tunaojiandaa kwenda kushiriki tena fainali hizo kama nchi mwalikwa kikosi kilichotajwa na kocha Salum Mayanga kimeonekana kuwagawa Watanzania kutokana na baadhi ya sura za kikosi hicho.

Taifa Stars itaenda kwenye michuano hiyo ikiwa na sura mpya za wachezaji Stamil Mbonde (mshambuliaji wa kati) na Amim Abdulkarim (mlinzi wa kushoto) ambapo baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka nchini wamepinga uteuzi wa nyota hao na kusema hawana sifa za kuichezea Taifa Stars kwa sasa.

Wachambuzi hao waliokataa kutajwa majina yao walikwenda mbali na kusema aina ya wachezaji hao walioteuliwa inakifanya kikosi hicho kionekane na sura za wachezaji wengi wa timu moja na tofauti na timu ya taifa iwe ya Watanzania wote.

“Unaweza kuona mchezaji kama yule mlinzi wa Toto Africans Abdulkarim ameitwa kikosini kutokana na uwepo wa kocha wake wa klabu yake (Fuljence Novatus) kuwa kwenye benchi la ufundi la Taifa Stars. Lakini ukitazama mchezaji mwenyewe hata ndani ya kikosi cha Toto Africans hakuwa akicheza mara kwa mara kutokana na uwepo wa mlinzi Salum Chuku ambaye hivi sasa amejiunga na Singida United.

“Uteuzi mwingine wa kushangaza ni ule wa Mbonde. Hivi tunatumia vigezo gani kuchagua mshambuliaji wa kuichezea timu ya taifa? Alihoji!

Mchambuzi huyo alisema nafasi ya Mbonde ingefaa kwenda kwa mshambuliaji wa Majimaji Kelvin Sabato (Kev Kiduku) aliyefunga mabao 10 katika mikikimiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyotoka kumalizika hivi karibuni” walisema.

Wachambuzi hao waliendelea kusema inastajabisha kuliona jina la kiungo wa zamani wa Mbeya City na sasa Singida United, Kenny Ally kwenye wachezaji 11 waliofanya vyema katika msimu wa ligi uliomalizika, lakini jina la kiungo huyo haliko kwenye kila kikosi cha timu ya taifa kinapoitwa.

“Nimewahi kucheza timu ya taifa kutokana na uwezo wangu ndani ya klabu. Ninachokifahamu mchezaji akifanya vyema kwenye timu yake kama anafaa kucheza timu ya taifa huyo anatakiwa kuitwa na kupewa nafasi, lakini kwa Yule nahodha wa Mbeya City na sasa kahamia Singida United (Kenny Ally) naona hadithi ya tofauti. Maana jina lake liko katika wachezaji 11 walioteuliwa na jopo la makocha wa ligi, lakini nashangaa jina lake haliko kwenye kikosi cha timu ya taifa” alisema.

Mwingine alidokeza kuwa “Aina hii ya uendeshaji wa soka unawagawa wachezaji ambao wanaona ili waweze kupata nafasi ya kucheza timu ya taifa wanatakiwa kuchezea timu fulani kitu ambacho si sahihi hata kidogo” aliongeza.

Kabla ya Mayanga kuteua jeshi lake la kwenda nalo Afrika Kusini kwenye michuano hiyo, lakini kocha huyo amekuwa akiwashangaza Watanzania aina ya wachezaji anaowaita kikosini.

Kitendo cha kuliona jina la mlinzi wa Azam, Erasto Nyoni katika vikosi vyake vya mara kwa mara ni kitu kingine kinachowashangaza Watanzania ambao wanahitaji kuona sura ya mkongwe Kelvin Yondan kwa ajili ya kusimama na vijana Abdi Banda, Salum Mbonde na Andrew Vicent (Dante).

Erasto si mchezaji wa kikosi cha kwanza wa Azam. Hali hii ndiyo inayofanya Watanzania washangae inakuwaje ndani ya klabu yake si mchezaji anayepata dakika nyingi, lakini timu ya taifa ni mlinzi tegemezi?

Inatajwa Yondani hana uhusiano mzuri na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kugomea safari ya Taifa Stars ilipokwenda Nigeria kucheza na timu hiyo ya taifa. Ushawishi wa Mayanga unahitajika kwenye eneo hili ili kumrejesha Yondani kikosini na iwe faida ya taifa na mchezaji mwenyewe.

Katika michuano hiyo ya COSAFA, Taifa Stars, imepangwa kundi A ambako wapinzani wake ni Mauritius, Malawi na Angola wakati Kundi B ni Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na Zimbabwe. Timu za Botswana, Zambia na Afrika Kusini kadhalika Namibia, Lesotho na Swaziland zitakuwa na mechi maalumu (play off) ili kuingia robo fainali.

Kikosi cha Mayanga kinaundwa na nyota Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Himid Mao, Erasto Nyoni na Shaban Iddy (Azam FC), Benno Kakolanya Hassan Ramadhan ‘Kessy’, Simon Msuva (Young Africans SC).

Said Mohamed (Nduda), Salum Mbonde na Stamil Mbonde (Mtibwa Sugar FC), Amim Abdulkarim (Toto Africans FC) Abdi Banda, Mzamiru Yassin, Shizza Kichuya (Simba SC),

Nurdin Chona (Tanzania Prisons), Salmin Hoza (Mbao FC) Raphael Daudi (Mbeya City) Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na Elius Maguli (Dhofar SC)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here