TAIFA STARS WAAPA KUISHANGAZA LIBYA

0
884

THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo inatarajia kushuka dimbani kuivaa Libya katika mchezo wa Kundi J wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2021), kwenye Uwanja wa Mustapha Ben Jannet, nchini Tunisia.

Mchezo huo unachezewa Tunisia badala ya Libya kutokana na hali ya machafuko inayoendelea nchini kwa wapinzani hao wa Tanzania.

Taifa Stars itakutana na Libya ikiwa imetoka kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Guinea ya Ikweta, katika mchezo uliochezwa Ijumaa iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Stars ambayo imepangwa kundi moja na Tunisia, Libya na Guinea ya Ikweta, inashika nafasi ya pili katika msimamo, ikijikusanyia pointi tatu baada ya kushuka dimbani mara moja.

Tunisia wanashika usukani wakiizidi Tanzania kwa idadi ya mabao, huku Libya ikiwa ya tatu na Guinea ya Ikweta ikiburuza mkia bila ya pointi yoyote.

Stars itashuka dimbani leo ikiwa na morali kubwa ya kutaka kuendeleza ubabe baada ya kupata ushindi katika mchezo uliopita.

Hata hivyo, Stars itamkosa mchezaji tegemeo wa kikosi hicho, Erasto Nyoni ambaye aliumia goti katika mchezo wa kwanza.

Macho na masikio ya Watanzani wote leo kuanzia saa 3:00 usiku, yataelekezwa kwenye Uwanja wa Mustapha Ben Jannet kuwashudia vijana wao wakifanya mambo.

Matumaini ya Watanzania ni kuiona timu yao hiyo inashinda mchezo huo ili kujitengenezea nafasi kubwa ya kufuzu michuano hiyo ya Afcon kwa mara ya tatu, baada ya kufanya hivyo mwaka 1980 ilipochezwa nchini Nigeria na mwaka huu Misri.

Kwa upande wao, Libya watashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya kupata kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Tunisia katika mchezo wao wa kwanza.

Kocha Mkuu wa Stars, Etienne Ndayiragije, ameuzungumzia mchezo wao wa leo akisema watacheza kwa kupambana kwa dakika zote 90, kuhakikisha wanatoka kifua mbele na kuendelea kuitangaza vema Tanzania.

“Matokeo yanapatikana katika uwanja wowote, iwe ugenini au nyumbani, hivyo sisi tumejiandaa kwa vyote, tutacheza kwa kujiamini ili tuweze kupata ushindi,” alisema.

Alisema wamewasoma wapinzani wao hivyo hana shaka ya kupata ushindi dhidi yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here