27 C
Dar es Salaam
Sunday, February 16, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Tafakuri Jadidi:Kwanini Mapinduzi, Kwanini Muungano?

Leo ni ‘ Mapinduzi Day’.
Ifahamike hapa, kuwa katika Zanzibar, Sherehe za Mapinduzi ndio sherehe kubwa kuliko zote ikiwamo za kiimani.

Shamrashamra za kuelekea siku ya leo huanza kwa shughuli mbalimbali za kwenye ratiba hata kabla ya mwaka mpya kuingia.

Bila shaka yeyote, Mapinduzi ya Zanzibar ni chimbuko pia la Muungano wetu.

Kwanini Mapinduzi?

Ndio, usiku wa kuamkia Januari 12 mwaka 1964, siku ya Jumapili, kama leo, ndio ilikuwa Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mapinduzi ya Zanzibar ni sura ya kipekee katika kitabu cha historia ya Bara hili. Ni mapinduzi yanayoshika rekodi duniani kuwa ni mafupi kufanyika na kukamilika kuliko yote duniani.

Nimepata kuandika, kuwa kwetu sisi wa Tanganyika, jambo la Zanzibar ni letu, imani hiyo pia iko visiwani, kuwa jambo la Tanganyika ni lao.Tuko jirani mno na tuna historia ya pamoja. Ni ndugu wa damu.

Nimepata kuwa Zanzibar mara nyingi. Nimepata nafasi ya kuongea na WaZanzibar. Nimedadisi Mapinduzi yale ya mwaka 1964. Nimedadisi Muungano wetu. Nimesoma pia maandiko ya wanazuoni wengi.

Na tujifunze kupitia historia. Nimeamini siku zote, kuwa historia ni Mwalimu Mzuri sana. Maana, hatuwezi kuyajua ya leo kama hatuyajui ya jana. Na hivyo, hatutoweza kupata mwanga kwa yatakayotokea kesho.

Shuleni nilipenda sana kusoma habari za Wanamapinduzi wa dunia hii. Kusoma habari za mapinduzi ya umma katika sehemu za dunia. Na si wengi wenye kufahamu, kuwa kuna tofauti ya mapinduzi na majaribio ya kuondoa Serikali madarakani. Hivyo, kuna tofauti ya revolution na coup d’etat.

Turudi Zanzibar, tangu nikiwa shule ya msingi, habari za Mapinduzi ya Zanzibar zilinivutia sana. Nilipata kusoma kitabu cha John Okello kilichonivutia sana. Kilihusu Mapinduzi ya Zanzibar. Kiliitwa ‘ Revolution In Zanzibar’.

Kupitia historia hiyo nilifahamu habari za wanamapinduzi wengine wa visiwani; ni watu wa aina ya Abdurahman Babu, Edington Kissasy, Kassim Hanga na wengineo.

Nilipomaliza Form Four pale Tambaza Secondary, nilifanya safari ya kwanza maishani mwangu kuvuka bahari. Safari ya kwenda Unguja. ( Pichani nikiwa Zanzibar, Januari, 1988)

Huko nilikuwapo wakati wa sherehe za Mapinduzi, Januari 12, 1988.

Naam, nilifurahia kuwapo mahala palipokuwa na vuguvugu la Mapinduzi ya mwaka 1964. Kuviona kwa macho na kutembea kwenye vitongoji vya Zanzibar; Mkunazini, Ziwani, Fuoni, Mji Mkongwe na kwengineko.

Mwandishi Ryszard Kapuchinski alikuwapo Dar es Salaam na Zanzibar wakati wa mapinduzi ya mwaka 1964. Kapuchinski anaandika; kuwa Karume alikuwa Dar es Salaam wakati mapinduzi yale yakiendelea kule visiwani.

Amemwelezea pia mtu aliyekuwa na control ya Mapinduzi kwenye field wakati Karume akiwa nje ya Zanzibar, ni John Okello aliyekuwa kijana wa miaka 25 tu.

Kapuchinski anamzungumzia Karume kama mtu aliyekuwa akiongea kwa sauti ya juu sana hata ukikaa nae karibu. Mara nyingi Karume alikuwapo pale New Africa Hotel, Dar Es Salaam, mahali walipokutana wanamapinduzi wengi wa bara hili.

” Pale juu New Afrca Hotel kulikuwa na baa watu wakiywa kahawa na vinywaji vingine. Hapo walikusanyika wanaharakati za kimapambano ya ukombozi wa Afrika kutoka kona mbalimbali.

Mahali hapa ilipangwa mikakati. Kwenye meza moja unaweza kumwona Edward Mondlane wa Frelimo akiongea na Keneth Kaunda wa UNIP. Meza nyingine unamwona Karume akiongea na Chisiza wa Malawi.
Katika ukanda huu Tanganyika ndio iliwatangulia wenzake kujikomboa.”- Ryszard Kapuscinski, Ebenholt ( Kwa Kiswidi) page 67-88)

Kwanini Muungano?

Ninapotafakari mitazamo tofauti juu ya dhana ya Mapinduzi ya Zanzibar, na kwa vile nimepata bahati ya kufika visiwani na kuongea na WaZazibar wa Mji Mkongwe na wa mashambani, kuna uhalisia ninaouona, kuwa suala la Zanzibar na hususan Muungano si jepesi kama wengine wanavyofikiri, au wanavyotutaka tufikiri.

Maana, Muungano ni zao la Mapinduzi ya 1964. Yale ya 1964 yalikuwa ni Mapinduzi ya Umma. Ni Mapinduzi ya Wajamaa wa Kiafrika. Ni muhimu watu wakajua historia sahihi ya Mapinduzi, lakini, yumkini swali muhimu leo si nani aliyewaongoza wakulima, wavuvi na wakwezi wale kufanya mapinduzi, bali, kuyafahamu malengo ya mapinduzi yale na kama yamefikiwa.

Naamini, kuwa kuuvunja Muungano leo ni kuvunja misingi ya uwepo wa Tanzania kama dola. Kuna hasara kidogo sana kubaki kwenye muungano, na hasara na madhara makubwa zaidi kuwa nje ya Muungano.

Zanzibar ya jana, leo na kesho, itabaki kuwa ni mkusanyiko wa wenyeji wa asili mbali mbali. Na wengi ni Waafrika wa kutokea Tanganyika. Mathalan, Zanzibar ina WaZanzibar wenye asili ya Unyamwezi, Usukuma, Umakonde, Uluguru, Uzaramo, Undengereko, Uarabu, Ushiraz na kadhalika.

Hivyo basi, swali gumu ni je, Mzanzibar ni nani nje ya Muungano?

Unafikiri haya unapokutana na Wazanzibar wenye kuongea Kinyamwezi lakini hawajawahi kukanyaga Sikonge wala Urambo, Tabora.

Mtafakari Mwalimu Nyerere aliposema mwaka ule wa 1964, kuwa kama ingewezekana, kuwa Mungu awezeshe Zanzibar isogezwe na upepo wa bahari na iwe mbali na Tanganyika, basi, huenda ingekuwa nafuu.

Naye Nyerere alikuwa akisumbuliwa na ukweli huo. Kuwa ni vigumu kwa Tanganyika kuondokana na Zanzibar katika uhalisia uliopo.

Maana, tulivyo sasa, suala la Zanzibar ni letu Tanganyika, na la Tanganyika ni la Zanzibar pia. Imekuwa hivyo jana, ndivyo ilivyo leo, daima itakuwa hivyo.

Yalikuwa malengo sahihi, ya waasisi wa Muungano, kuwa uanze na Serikali MBILI kwa lengo la kwenda kwenye Serikali MOJA. Na kuunganisha vyama; Afro Shiraz na TANU ulikuwa ni mwanzo wa safari ya kuelekea kwenye kuyafikia malengo hayo.

Maana, Serikali kibaraka ya Sultan iliyopinduliwa mwaka 1964 ( Yale ni mapinduzi, si coup d’etat kama wengine wanavyopotosha) haikuwa na malengo ya kuukomboa umma wa Zanzibar ulio na mchanganyiko wa hata wenye asili ya Bara. Serikali iliyoundwa na ZNP na ZPPP ilikuwa ni mabaki ya Usultani ambao wanyonge walio wengi visiwani hawakuwa na faida nao.

Huu ni wakati wa kujitafakari. Ni wakati wa kujisahihisha pia. Kuyaacha malengo ya waasisi ya kuufikia Muungano Kamili wa Serikali MOJA kutoka kwenye Serikali MBILI, na kubadili mwelekeo kwenda kwenye Serikali TATU, kimsingi itakuwa ni kuianza safari ya kurudi Tanganyika na Zanzibar pasipo MUUNGANO.

Historia inatufundisha nini?

Itakumbukwa baada ya Vita Kuu ya Pili, dunia ilipitia kipindi cha vita baridi . Miaka ile ya 60 dunia iligawanyika katika kambi mbili kubwa kiitikadi; zilijulikana kama Warsaw Pact na Nato Pact. Kambi ya Warsaw iliongozwa na Urusi ya zamani na ile ya NATO iliongozwa na Marekani.

Kulikuwepo pia na kundi la nchi zisizofungamana na upande wowote. Tanzania ilikuwa mwanachama wa kundi hili. Hata hivyo, nyingi ya nchi hizi kimsingi zilikuwa na upande zilizoegemea kati ya makundi mawili niliyoyataja.

Tunasoma kuwa Marekani na hususan kupitia Shirika lake la ujasusi la CIA, ilijiingiza kwa mara ya kwanza katika siasa za Zanzibar mara baada ya mapinduzi ya 1964. Ni kwa lengo la kupunguza kasi ya kuenea kwa Ukomunisti.

Marekani iliingiwa na hofu ya Zanzibar kama kisiwa kutumiwa na Wakomunisti. Katika Zanzibar bado kuna kumbukumbu ya historia hii kwa kuyaangalia majina kama Uwanja wa Mao Tse Tung, Hospital ya V.I Lenin, shule za Fidel Castro, Patrice Lumumba na mengineyo. Yote haya yalikuwa na mwelekeo wa kambi ya Warsaw; Ukomunisti.

Mvutano wa kiitikadi kati ya Warsaw na NATO uliendelea kuwepo hadi pale ukuta wa Berlin uliopoangushwa Agosti 23, 1989. Huo ndio ulikuwa mwisho wa vita baridi ya dunia. Marekani ikabaki bila mpinzani wa kiitikadi. Kuanzia hapo upepo wa kisiasa uligeuka ghafla, wimbi la demokrasia ya vyama vingi likaanzia Ulaya Mashariki na kuikumba Afrika.

Kati ya mwaka 1990 hadi 1998 tulishuhudia kuwepo kwa ombwe la kiitikadi. Uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 1995 ulifanyika kukiwa na ombwe hilo la kiitikadi duniani.

Miaka mitatu baadae, Agosti 7, 1998, sura ya dunia ilianza kubadilika tena . Ni mara ile balozi za Marekani Nairobi na Dar Es Salaam zilipolipuliwa. Septemba 11, 2001 sura ya dunia ilibadilika ghafla, pale kikundi cha kigaidi cha Alqaida kilipofanya maangamizi makubwa katika miji ya Washington na New York.

Hii Ni Tafakuri Jadidi.

Happy Mapinduzi Day!

Maggid Mjengwa,

Jambiani, Kusini Unguja, Zanzibar.
Jumapili, Januari 12, 2025.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
594,000SubscribersSubscribe

Latest Articles