28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

TAFADHALINI MALAIKA MSIZIME MITANDAO YA KIJAMII

Rais Dk. Magufuli akifurahia jambo wakati akiwa ndani ya basi la Mwendokasi pamoja na
Rais wa Benki ya Dunia, Dk. Jimmy Young, kabla ya kuzindua mradi wa ujenzi wa Ubungo
Interchange.

 

 

NA MARKUS MPANGALA

MATAMSHI mawili yaliyotolewa na Rais John Magufuli katika matukio mawili tofauti yamekuwa yakinifikirisha mno. Mosi, matamshi ya kutaka Malaika ashuke ili azime mitandao ya kijamii kusaidia watu wafanye kazi kwa utulivu yaliyotolewa na Rais wetu mnamo Septemba mwaka jana wakati wa uzinduzi wa ndege mbili za Serikali zilizonunuliwa nchini Canada aina ya Bombardier Q400.

Rais Magufuli alisema haya: “Natamani Malaika ashuke azime mitandao ya kijamii baada ya mwaka mmoja ikute hatua kubwa za kimaendeleo tulizopiga”.

Pili,  Machi 17, mwaka huu, Rais Magufuli akizungumza wakati wa  kuweka jiwe la msingi katika mradi wa barabara za juu (Flyovers) Ubungo,  mkoani Dar es Salaam, alisema: “Watu wa Dar es Salaam tumejielekeza sana kwenye udaku ambao hausaidii maendeleo. Udaku ambao haumalizi hata foleni ya Dar.

“Ningefurahi sana huko kwenye mitandao kama tungekuwa tunajadili jinsi ya kufanya mambo ya maendeleo. Mimi sionyeshwi njia ya kupita na mtu. Njia ya kupita tayari nilishaonyeshwa na ilani ya chama changu. Kuandikwa kwenye mitandao hata mimi ninaandikwa, kwa hiyo nijiuzulu? Kuandikwa kwangu mimi siyo tija bali kuchapa kazi.

“Kuna wengine mmefikia hata hatua ya kunipangia. Nasema mimi ukinipangia ndio umeharibu. Vitu ambavyo havina msingi vinachukua muda wetu mwingi sana. Mara uposti hiki, mara uweke kile. Watanzania mjue kampeni zimeshakwisha. Ulie, ugaregare lakini Rais ni mimi John Pombe Magufuli na kwangu ni kazi tu.

“Mimi ni rais ninayejiamini, sipangiwi mambo ya kufanya. Hata fomu ya kugombea nilikwenda kuichukua peke yangu, kwa hiyo Makonda wewe chapa kazi,” amesema Rais Magufuli.

Baada ya kupitia kauli hizo mbili, ninapata jawabu kuwa bado kuna mtazamo hasi dhidi ya mitandao ya kijamii mbele ya Rais. Mtazamo hasi umejikita pia kwa baadhi ya kizazi kilichozaliwa kabla ya ukoloni na baadaye ukoloni, hususan kuanzia miaka 1969 kushuka chini.

Angalau waliozaliwa miaka 1970 kwenda juu wanaweza kuwa na mtazamo chanya juu ya mitandao ya kijamii. Kumekuwa na wimbi la kuchukizwa ama kuiona mitandao hiyo kama ‘dudu’ lisilo na tija. Mtazamo wa aina hii ndio unatafsiri kuwa mitandao ya kijamii hakuna cha mno au imekuwa sehemu ambayo watu hawajadili wala kufanya mambo ya maana katika maisha yao.

Ninaweka ‘veto’ katika mitazamo hasi dhidi ya mitandao ya kijamii. Ninazo sababu za kuthibitisha mbele ya Rais au hata viongozi na wananchi wote ambao wanaitazama mitandao ya kijamii kama ‘takataka’.

Kutokana na umuhimu wa mitandao hii ingelifaa kizazi hiki chenye kuitazama kama ‘takataka’ ni vema kuonyeshwa mambo muhimu ama vitu vinavyofanyika, na kuchangia ulipaji wa kodi pamoja na ukusanyaji wa mapato kwenye mamlaka zinazohusika.

Mkononi ninacho kitabu cha “The Accidental Billionaires: The Founding of Facebook: A Tale of Sex, Money, Genius and Betrayal,” kilichoandikwa na Ben Mezric. Ingawaje sijaanza kukisoma, lakini ninao ufahamu namna mwanzilishi wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mark ZuckZuckerberg alivyofanikiwa kuwa bilionea. Namna alivyoajiri Wamarekani wenzake na raia wa kigeni.

Kwahiyo mitandao ya kijamii tunazungumzia ‘uvumbuzi’. Tunazungumzia ubunifu kazini na namna inavyoweza kuleta tafsiri mpya ya utendaji wa kazi.

Mitandao ya kijamii ni fedha. Mitandao ya kijamii imeajiri watu. Mitandao ya kijamii imetupatia ujuzi wa kuwa madalali wa bidhaa mbalimbali na kujiongezea kipato na kulipa kodi. Mitandao ya kijamii imekutanisha watu waliopoteana, ndugu na marafiki.

Mashirika mbalimbali yana kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii ili kuwafikia wateja wao popote walipo na inaendeshwa na waajiriwa rasmi. Kuna benki, asasi za kiraia, vyombo vya habari, historia, skolashipu, vyuo vikuu na taasisi za elimu, masomo na biashara mbalimbali.

Mitandao ya kijamii inao wataalamu wake, walioketi darasani na kufuzu. Mitandao ya kijamii ni maendeleo ya uchumi. Mitandao ya kijamii imerahisisha matangazo ya biashara zao kwa urahisi mno.

Mitandao ya kijamii inarahisisha dhana ya upashanaji wa habari na mawasiliano. Hatutakiwi kurudi zama za matumizi ya Yahoo Messenger, Google Chart, Hotmail, Dar Hotwire, Marafiki.com, Tagged n.k.

Kwenye mitandao ya kijamii tulianzia zama za vikusanya habari (Aggregators) ya kampuni ya Goolge (Blogger) hadi kwenye huduma za habari (News Feed) ya bilionea wa Facebook au waanzislihi wa Twitter, Jack Dorsey, Noah Glass, Biz Stone na Evan Williams mnamo mwaka 2006.

Mitandao ya kijamii tunapigiana simu za video, tunaongea mubashara na rafiki zetu, tunakuza mapato ya kampuni za simu kote nchini. Hatutakiwi kurejea zama za barua za kubebwa na tarishi au mpaka sanduku la posta.

Hatutakiwi kurudi zama za simu za mikorogo. Hatuhitaji kurudi zama za kompyuta za mwaka 1974 ambazo zilikuwa kubwa kama meza. Ndiyo maana tunasema hizi ni zama za habari (Information Age).

Habari ni biashara. Kila mwananchi ni ripota wa mtaani kwake. Anaripoti yanayojiri. Kila mwananchi anaweza kutengeneza vipindi vyake vya runinga akiwa ‘Live’ kupitia Facebook, Twitter, Blogu, au WhatsApp.

Mitandao ya kijamii inachangia ulipaji kodi. Taswira ya mitandao ya kijamii siyo umbeya pekee. Ni uchumi na maendeleo. Ni vyanzo vya habari kwa majasusi wa idara za usalama ulimwenguni.

Mwaka 2006 Mwanablogu bora Afrika na wa kwanza kublogu kwa lugha ya Kiswahili, Ndesanjo Macha, alipata kusema Blogu siyo upepo wa kupita. Naamini aliunganisha na mitandao ya kijamii si jambo la kupita.

Kuikasirikia mitandao ya kijamii ni sawa na kupunguza chanzo cha mapato (kodi). Upande wa pili wa mitandao ya kijamii faida ni nyingi. Tuikague elimu yetu. Tujiulize kwanini hapa nchini wavumbuzi wa Magobore tunawafunga gerezani badala ya kuwatumia wavumbue vitu kama walivyofanya wenzetu wa mitandao ya kijamii. Hapa kwetu tumefuta somo la kilimo, wakati ndicho uti wa mgongo.Vituko hivi!

Baruapepe; [email protected]

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles