21.9 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

TAEC yavifungia vituo vitatu kutoa huduma ya X-ray kwa kukiuka sheria

Mwandishi Wetu, Mwanza

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imevifungia vituo vitatu vya afya jijini hapa kutoa huduma ya mionzi (X-ray) kutokana na  kutokidhi matakwa ya Sheria.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TAEC, Peter Ngamilo amesema vituo hivyo vimekiuka Sheria Na. 7 ya Nguvu za Atomiki ya Mwaka 2003, kifungu namba 12, ambacho kinazuia mtu asiye mtaalamu wa kupiga picha za mionzi kufanya hivyo.

Amesema katika baadhi ya vituo hakukuwa na wapiga picha za mionzi na vifaa vyenye ubora na kwamba vitarejeshewa huduma hiyo mara vitakaporekebisha mapungufu yaliyoonekana.

Amevitaja vituo vilivyofungiwa kutoa huduma hiyo kuwa ni Hospitali Teule ya Wilaya ya Sumve, Hospitali ya Wilaya ya Ngudu na Hospitali  ya Wilaya ya Misungwi.

“Vituo hivyo vimefungwa huduma ya hiyo wakati wa ukaguzi unaoendelea mkoani Mwanza ikiwa ni zoezi linalofanyika kila mwaka katika kuhakikisha usalama wa utoaji wa huduma ya mionzi unafuatwa kama ambavyo  ilivyoelekezwa katika Sheria Na. 7 ya Nguvu za Atomiki Tanzania ya Mwaka 2003 ili kulinda wafanyakazi, wagonjwa, wananchi na mazingira dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi.

“Katika vituo vya Sumve na Ngudu imegundulika kuwa watumishi wake hawana sifa za upigaji picha za mionzi huku katika kituo cha Misungwi imegundulika kuwa vifaa vyao vya mionzi havina ubora unaostahili.

“TAEC inavitaka vituo vyote vinavyotumia mionzi katika utoaji wao wa huduma mbalimbali kuhakikisha vinafuata Sheria na taratibu za  kiusalama kama ilivyoelekzwa katika sheria ikiwemo kuishirikisha TAEC katika hatua zote za ujenzi wa vituo hivyo kwa lengo la kulinda afya za Watanzania,” amesema.

Wakati huo huo katika ukaguzi huo unaoendelea mkoani humo, jumla ya vituo 32 vimekaguliwa ambapo vituo 28 ni vya sekta ya afya na vituo vinne ni katika sekta ya viwanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,719FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles