24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TADB KUENDELEZA KILIMO BIASHARA NA MAFUNZO

Na George Mshana,

Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imekopesha wakulima 2575 mwaka huu kutoka 944 mwaka jana.

Benki imekopesha kutoka Sh 1.0 bilioni hadi Sh 6.5 bilioni na benki imeweza kukopesha vikundi vinane (8) hadi vikundi 20.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa benki  hiyo, Francis Assenga, katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa wiki iliyopita  jijini Dar es Salaam.

“Benki imeweza kuvijengea uwezo vikundi 336 vya wakulima wadogo wadogo vyenye jumla ya wanachama 44,400 katika mikoa ya Iringa, Morogoro na Tanga. Hivyo kuwezesha jumla ya vikundi 19 kutimiza masharti na maandalizi ya msingi ya kuweza kukopa; vikundi vingine vilivyobaki vinaendelea kupatiwa mafunzo ili viweze kufikia hali ya kuweza kukopesheka.

Mafunzo na semina kwa wadau mbalimbali wa kilimo yanaendelea kutolewa na benki kwa wakulima, viongozi wa vikundi na taasisi pamoja na washirika mbalimbali,” anasema Assenga.

Serikali ikishirikiana na TADB imefanya mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na kupelekea Bodi ya Benki ya Maendeleo Afrika kutoa kibali cha kuipatia TADB fedha za kukopesha kwenye sekta ya kilimo.

Mkataba wa mkopo umesainiwa Desemba mwaka jana kati ya AfDB na Wizara ya Fedha na Mipango, ambapo TADB inatarajiwa kupatiwa fedha zaidi ya billion 200 kwa ajili ya kukopesha wakulima.

Assenga anasema  benki imepitia upya mpango mkakati wake katika kutoa mikopo ili kufikia wakopaji wengi zaidi na kufikia lengo la kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo.

Mambo muhimu ya kimkakati yaliyopitiwa upya ni pamoja na; kuongeza eneo la kijiografia; bidhaa na huduma zitolewazo; utaratibu wa utoaji mikopo na minyororo ya thamani ya kipaumbele.

Assenga anasema benki itaboresha huduma kwa kuanzisha mazao maalumu ya huduma za kibenki kwa wakulima wadogo wadogo kulingana na mnyororo husika wa thamani na pia kuboresha huduma kupitia taasisi za fedha zilizopo ili kufikia wakulima wengi zaidi.

Anaongeza kuwa benki hiyo imepanga kupanua wigo wa eneo la huduma na kufika nchi nzima ambapo ofisi sita za kanda na mikoa zitafunguliwa, ili kuongeza ufanisi katika utoaji kwa huduma kwa wateja.

Assenga anasema benki inatoa mikopo ya kuendeleza miradi ya kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yaliyoainishwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na kutanuka nchi nzima kwa utaratibu mahsusi.

Anasema benki itawajengea uwezo wafanyakazi wa TADB, mabenki mengine na wadau mbalimbali wa kilimo hususan wale watakaoshiriki katika hatua mbalimbali za mchakato wa kutoa mikopo.

Lengo ni kuchagiza jukumu la TADB la kuwa benki kiongozi ya maendeleo ya kilimo pamoja na kuhamasisha mabenki na taasisi nyingine za kifedha kutoa fedha kwenye mnyororo mzima wa kilimo.

Assenga anaongeza kuwa mkakati mwingine ni kuitangaza benki na huduma zake kwa wananchi ili wengi waweze kuzielewa shughuli zake na jinsi benki itakavyowahudumia.

Benki itasimamia utoaji na usimamizi wa fedha kwenye uendeshaji wa miradi ya kilimo mbalimbali nchini.

Anabainisha kuwa benki itaratibu upatikanaji wa dhamana mbalimbali kwa ajili ya mikopo kwa wakulima ili mabenki yaweze kuelekeza nguvu zao kuwakopesha wakulima wengi zaidi.

Benki itafanya upembuzi wa miradi ya maendeleo ya kilimo na umwagiliaji nchi nzima ili kubaini mahitaji halisi ya fedha na pia kusaidia kupanga maeneo ya vipaumbele.

Assenga anasema benki itafadhili miradi ya umwagiliaji isiyopungua 20 na teknolojia mbadala tatu kwa maeneo yatakayoainishwa.

Anaongeza kuwa enki itakopesha mashamba makubwa yasiyopungua 10 yatakayosaidia kuinua wakulima wadogo wadogo  kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara.

Anasema pia benki itatoa mikopo kwa wakulima wadogo wadogo walau laki tano watoke kwenye kilimo cha kujikimu.

“Benki itasaidia uanzishaji wa biashara za kilimo za vijana zisizopungua 1,000 na kuendesha programu za mafunzo 50 kwa vijana,” anasema.

Anasema benki itafadhili ujenzi wa maghala ya kimkakati katika kila kanda kubwa ya uzalishaji wa mazao ya nafaka.

Anaongeza kuwa benki itaendesha mafunzo kwa taasisi za fedha zisizopungua 20, taasisi za kutoa mikopo 300 na vikundi vya wakulima wadogo wadogo 1,000.

“Benki itafungua matawi ya benki katika kila kanda yaani kanda sita (6) ikiwemo Zanzibar hadi 2020,” anasema Assenga.

Assenga anazitaja changamoto zinazoikabili benki hiyo katika utoaji wa mikopo kuwa ni pamoja; kutokuwa na mvua za uhakika ukizingatia kuwa wakulima wengi wadogo wadogo wamekuwa wakilima kilimo cha kutegemea mvua.

Pia uelewa mdogo wa taratibu za kibenki kwa viongozi wa vyama vya wakulima wadogo wadogo pamoja na wanachama wanufaika wa mikopo.

Anaongeza kuwa uelewa mdogo juu ya kanuni za kilimo bora ikiwa ni pamoja na upungufu wa huduma za ugani zitolewazo kwa wakulima wadogo wadogo.

Pia, kukosekana kwa masoko ya uhakika kwa wakulima wadogo wadogo, ambapo wanunuzi wengi wakubwa wamekuwa wakisita kusaini mikataba ya ununuzi wa mazao ili kutoa soko la uhakika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles