26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Tacaids wataja umri hatari vijana kupata VVU

MWANDISHI WETU –Dar es Salaam

MKURUGENZI Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk. Leonard Maboko, amesema sababu za vijana kuongezeka kwenye maambukizi mapya ya Ukimwi ni kutopata elimu wakati wa kutoka katika utoto kwenda ujana.

Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mipango ya mfuko wa kudhibiti Ukimwi.

 “Hawajapata elimu (vijana) sawasawa, hivyo inakuwa rahisi kufanya maamuzi ambayo hana taarifa za kutosha. Lakini pia vijana wa kike kutaka kupata vitu kwa haraka.

“Ndiyo maana tuna miradi ambayo inagusa kaya masikini kwa kuwasaidia kupata elimu ya ujasiriamali katika mikoa mitatu,” alisema.

Alisema hadi sasa Tanzania inao watu milioni 1.5 wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi ambao ni sawa na asilimia 4.7.

“Lakini maambukizo mapya yamepungua kutoka 80,000 miaka minne iliyopita hadi 72,000. Katika kundi hili Watanzania 6,000 wanapata maambukizo mapya kwa mwezi na kwa siku ni 200.

“Pia kati ya watu 200, vijana 80 wenye umri wa miaka 15 hadi 24 pia huambukizwa kwa siku,” alisema.

Alisema tatizo la ugonjwa wa Ukimwi linabadilika kila mara, hivyo kuchangia zaidi ya asilimia 40 ya vijana kuathiriwa huku asilimia 80 wakiwa ni wasichana.

Katika hatua nyingine, Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM) kupitia mfuko maalumu wa Kili Challenge, umetoa wito kwa asasi za kiraia zinazotoa huduma za Ukimwi nchini, kuandaa andiko kuomba fedha zilizochangwa na kampuni hiyo kupitia wadau.

Meneja wa Kili Challenge, Manase Ndoroma, alisema Bodi ya Kili Challenge ilikaa na kuamua Sh milioni 800 ambazo kati yake Sh milioni 550 zitabakia kusubiri asasi mbalimbali zitakazowasilisha maombi yao kuomba fedha hizo.

 “Sh milioni 150 zitaenda Tacaids kujenga vituo vinavyotoa huduma za Ukimwi, Sh milioni 50 zinatolewa kwa kituo cha kulea watoto yatima mkoani Geita – Moyo wa Huruma Orphanage Center kukiwezesha kiuchumi, Sh milioni 50 zitakwenda kwa Mfuko wa Ukimwi (ATF) wakati Sh bilioni 1.173 zilizotolewa na GGM zitaenda Tacaids,” alisema Ndoroma.

Alisema Kili Challenge ni mfuko unaoratibiwa na GGM na Tacaids kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuchangisha fedha kwa kupanda Mlima Kilimanjaro na hupelekwa kusaidia kutoa huduma za kutokomeza maambukizi ya VVU/Ukimwi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles