24.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

TACAIDS: Wanaume wa umri miaka 50-54 wanaongoza maambukizi ya VVU

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital-Morogoro

Wanaume wenye umri wa miaka 50 hadi 54 wanaongoza kwa kiwango cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini Tanzania, kwa mujibu wa taarifa kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS). Kwa upande wa wanawake, kinamama wenye umri wa miaka 45 hadi 49 ndiyo walioathirika zaidi, huku wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wakiwa katika hatari kubwa zaidi ya maambukizi mapya ya VVU kitaifa.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Jerome Kamwela, alieleza hayo Mei 29, 2024 mjini Morogoro wakati wa semina iliyowalenga wahariri na waandishi wa habari kuhusu hali ya maambukizi ya VVU, unyanyapaa, Sheria ya Ukimwi, na mbinu bora za vyombo vya habari katika kutoa elimu ya kujikinga na VVU kwa vijana.

Dk. Kamwela alifafanua kuwa, kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni wa Ukimwi (THIS 2022/23), Tanzania ina watu 1,548,000 wanaoishi na VVU (WAVIU). Aliongeza kuwa, kiwango cha maambukizi mapya kwa watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 15 kimepungua kwa asilimia 16.7, kutoka maambukizi 72,000 (THIS 2016/17) hadi 60,000 (THIS 2022/23). Hata hivyo, alionya kuwa maambukizi mapya ya VVU yameongezeka maradufu kwa wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 24.

“Utafiti unaonesha kuwa maambukizi mapya yamepungua kwa wanaume wa rika zote (watoto na watu wazima) na kwa wanawake watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 15. Lakini, ushamiri wa VVU kwa watu wazima (15+) ni wa asilimia 4.5, ambapo ni asilimia 5.6 kwa wanawake na asilimia 3 kwa wanaume,” alisema Dk. Kamwela.

Kwa upande wa mikoa, Dk. Kamwela alibainisha kuwa ushamiri wa VVU unatofautiana kutoka asilimia 1.7 katika Mkoa wa Kigoma (kiwango cha chini) hadi asilimia 12.7 katika Mkoa wa Njombe (kiwango cha juu zaidi). Alitaja mikoa ya Njombe, Iringa, na Mbeya kuwa juu ya wastani wa kitaifa wa ushamiri wa VVU wa asilimia tisa.

Akizungumzia utekelezaji wa malengo ya kimataifa ya “95-95-95” ifikapo mwaka 2025, Dk. Kamwela alisema Tanzania imeshafanikiwa kufikia lengo la pili, ambalo linahusisha asilimia 95 ya WAVIU wanaojua hali zao kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU. Hata hivyo, alisema kuwa Tanzania bado iko nyuma katika kufikia lengo la kwanza, ambapo ni asilimia 78 tu ya watu wazima wenye VVU wanajua hali zao. Aliwataka wanaume na vijana kuongeza juhudi katika kupima afya zao ili kufanikisha malengo hayo.

Dk. Kamwela alitoa mtazamo tofauti kuhusu mikoa ya Njombe, Iringa, na Mbeya, ambayo inaonekana kuwa na ushamiri mkubwa wa VVU. Alisema kuwa, ingawa mikoa hiyo ina viwango vya juu vya ushamiri, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kupunguza makali ya VVU kwa WAVIU, hivyo kusababisha idadi ndogo ya vifo na kuifanya mikoa hiyo kuonekana kuwa na idadi kubwa ya WAVIU.

Kwa mfano, Mkoa wa Njombe una ushamiri wa asilimia 11.6 kwa wanaume na asilimia 12.7 kwa wanawake, lakini umefanikiwa kupunguza makali ya VVU kwa asilimia 60.5 kwa wanaume na asilimia 86.7 kwa wanawake. Hali kama hiyo imeonekana katika Mikoa ya Iringa na Mbeya.

Dk. Kamwela pia alitoa wito kwa wadau mbalimbali kuchangia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi badala ya kutegemea ufadhili kutoka nje ya nchi. Alisema kuwa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonesha kuwa asilimia 60 ya WAVIU wako Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, na changamoto kubwa ni hali duni ya maisha katika eneo hilo.

“Ufadhili kutoka kwa mataifa makubwa kiuchumi umeelekezwa zaidi kwenye miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ni wakati sasa Afrika tukubaliane kuwekeza fedha zetu za ndani kulinda watu wetu dhidi ya VVU/Ukimwi,” alisema.

Pia alitoa angalizo kuwa, kadri maeneo yanavyokua kiuchumi au kupata miradi mipya ya maendeleo, ndivyo ongezeko la maambukizi ya VVU linavyoongezeka, akitoa mifano ya Mikoa ya Dodoma na Tanga ambapo ongezeko la miradi mikubwa limeambatana na ongezeko la maambukizi ya VVU.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles