25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Taboa:Tumefikia pazuri mfumo wa kielektroniki

LEONARD MANG’OHADAR ES SALAAM

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), kimesema kimefikia hatua nzuri za kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa kukata tiketi kama ilivyoagizwa na Serikali.

Akitoa maazimio ya mkutano mkuu wa chama hicho ulioketi Dar es Salaam juzi, Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, alizitaja baadhi ya hatua zilizofikiwa ili kuanza kutumia mfumo huo kuwa ni pamoja na kupata kampuni tano zitakazotoa huduma katika kanda tano.

Alisema leo wanatarajiwa kukaa na watoa huduma  ili kujadiliana kuhusu bei watakayowatoza kutokana na wanachama kudai  gharama ya asilimia 0.7, bado ni kubwa na baada ya hapo watoa huduma hao watakwenda mikoani kutoa elimu kwa watumiaji wa mfumo.

“Hatuhitaji kuletewa mtu, sisi ni taasisi huru ambayo inaheshimika na tuna mamlaka yetu. Tumeshapata ‘venders’ wetu tayari kwa kila kanda kwa hiyo kama kuna mtu mwingine atapata watu wake wengine aendelee na hao.

“Tumesema tunataka kuunganishwa na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kupunguza gharama hatutataka kuunganishwa kwa mtu mwingine akatutoze. Kama mlivyosikia chaji watu wamekwenda hadi asilimia 0.7,bado wanataka ipunguzwe kidogo ili tuweze kuanza kazi.

Alisema wamekubaliana na watoa huduma hao kuwa ndani ya siku 45 kila kitu kitakuwa tayari ikiwamo kuingiza mashine za kukatishia tiketi (POS) pamoja na kutoa mafunzo.

Alisema bei ya POS, itakuwa Sh 250,000 ambazo zinaweza kutolewa kwa kukopeshwa  mmiliki kulipia kidogo kidogo, kukodisha au kununua kwa fedha taslimu na kwamba wameamua kufanya hivyo ili taifa lisikie wameshatoka hatua moja kwenda nyingine.

“Tusingetaka tusikie kwamba tunasukumwa au tunalazimishwa hatua tuliyofikia ni nzuri hatutaki tena turumbane na serikali, Jumatatu tunafanya makubaliano ya mwisho kisha tunaingia kwenye mikataba yetu na kuendelea na kazi.

Kuhusu kuwapo taarifa kuwa kesho Latra wanamtangaza mtoa huduma mwingine kwaajili ya kuendesha mfumo wa kukatisha tiketi hizo alisema kuwa wanachotambua ni kwamba Latra ni mdhibiti wa Usafiri na hata katika kanuni zake hakuna mahala inawabana wao wafanye kazi na mtu Fulani.

“Wamiliki tuko huru kuchagua mfumo, tunayo barua ya TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), inayotutaka tupeleke watu wenye mfumo, sasa huyo atakayetukatalia kwamba sisi lazima tuingie huko alikotangaza hao waliobaki nje ya mfumo ambao si wanachama wetu wana uhuru wa kujiunga popote, lakini sisi tayari tumeshapata mfumo wetu hatutaki kujiunga na mtu yeyote.

Kuhusu usalama wa fedha zao wamesema kuwa suala hilo litaingizwa kwenye mkataba na kwamba moja ya masharti ni lazima mkandarasi anayepewa kazi hiyo awe na uwezo wa kifedha ili ikitokea amepoteza fedha zao awe na uwezo wa kuzilipa.

Alisema  katika makubaliano yao watoa huduma hao watagawanywa katika kanda tano ambazo ni pamoja na Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Kaskazini, Kanda ya Ziwa na kanda ya Kati

Alisema  licha ya Juni 30, mwaka jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  kuagiza TRA ikae na chama hicho ili kushughulikia suala hilo haijaweza kufanya hivyo badala yake wamekuwa wakilaumiwa kuwa hawataki kutumia tiketi za kielektroniki.

Kuhusu mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTS) alisema umeendelea kuwavuruga  na kwamba wanachama wameamua kuwa kwa kuwa Waziri Mkuu ndiye aliyesitisha tozo zilizokuwa zinatozwa na kambuni zilizokuwa zinafunga mifumo hiyo, wanataka wapate barua kutoka ofisi ya Waziri Mkuu ili wajue kama gharama hiyo imeshuka ili waweze kuendeelea kufunga na kulipia.

Kuhusu baadhi ya kanuni za sheria ya Latra ambazo hazitekelezeki ikiwamo kumtaka mmiliki wa basi kuweza alama kwenye mzigo yote inayobebwa kwenye basi alisema kuwa wameazimia kutumia njia tatu kumaliza suala hilo ikiwamo kuandika barua kwenda katika mamlaka husika, kutumia njia za kisiasa na ikishindikana wasitishe kutoa huduma.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles