26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tabia za mtoto anazorithi kutoka kwa wazazi

Na MWANDISHI WETU

KUNA tabia fulani tunaweza kuwa nazo ambazo, kwa hakika, tunajua zinatufananisha na wazazi wetu. Tunafanya vitu fulani, wakati mwingine bila hata kujua, lakini vinafanana na yale tuliyowahi kuwaona wazazi wetu wakiyafanya. 

Ipo mifano mingi kuelezea jambo hili. Baba, kwa mfano, unaweza kuwa na tabia ya hasira kali. Mwanao akifanya kosa dogo unakuwa mwepesi wa kukemea. Wakati mwingine, unatoa adhabu kubwa mno zisizolingana na makosa halisi ya mtoto. Ukichunguza vizuri unakuta kumbe ndivyo alivyo na baba yako. 

Kwamba, baba yako pengine alikuwa na tabia ya kufoka mara kwa mara hata kwa mambo ambayo kwa hali ya kawaida ni madogo. Wewe wakati huo ukiwa mdogo hukupenda kumwona mzazi wako akifoka hadharani. Sasa hivi bila kujielewa unajikuta na wewe unayafanya yale yale ambayo hukupenda kuyaona kama mtoto. 

Wapo wazazi ambao ni wepesi kuchapa watoto. Wanafanya hivyo wakifikiri wanawasaidia kujenga tabia njema. Si kwamba wazazi hawa wanapenda kuwachapa watoto wao. Hapana. Kimsingi, hata wao walipokuwa watoto hawakupenda kuchapwa. Waliogopa. Leo wamekuwa wazazi wanakuwa wepesi kuchapa. 

Mwanao anaweza kufanya kosa dogo. Ungeweza kabisa kulipuuza au kulitatua kwa njia ya kirafiki. Lakini bila hata kujua sababu, unajikuta umemfokea, umemchapa na hata kumdhalilisha. Hasira zikipoa baadae, unajilaumu kwanini umefanya hicho ulichokifanya. 

Si kwa watoto pekee. Inaweza kuwa hata kwa mwenzi wako. Unaweza kutamani kabisa kuongea kwa lugha ya kistaarabu kwa mpenzi wako, lakini unajikuta unafoka na kulalamika. Unatamani maisha fulani ya ukaribu lakini hufanyi. Kila unapojaribu, nafsi inakuwa kama inakuzuia kutekeleza jema unalolijua. Badala yake unashangaa unamfanyia baya usilolikusudia unalokuja kulijutia baadae.

Aidha, inaweza pia kuwa kwa wazazi wako mwenyewe. Unatamani kuwatendea wema wazazi wako lakini huwezi. Unatamani ungekuwa karibu nao, uongee nao kwa nidhamu lakini moyo wako unakuwa mzito. Ni kama unaishi na uchungu fulani dhidi ya wazazi wako ambao kimsingi huelewi chanzo chake. 

Utoto unaoishi ndani yetu 

Wataalamu wengi wa saikolojia wamejaribu kuchunguza jambo hili. Katika tafiti zao wamejaribu kujua kwanini wakati mwingine tunafanya mambo tusiyoyakusudia. Kwamba, tunashindwa kufanya mazuri tunayotaka lakini tunafanya mabaya tusiyoyakusudia. 

Upo ushahidi wa kutosha kuwa matukio anayokutana nayo mtu tangu akiwa tumboni mwa mama yake yanayo nguvu kubwa ya kuamua mustakabali wake. Matukio yanayotupata katika umri mdogo yanatuumba kuwa vile tutakavyokuwa ukubwani. 

Kwa mfano; inawezekana wazazi wako walipigana mbele yako ulipokuwa na umri wa miaka miwili. Katika umri huo, hukumbuki kilichotokea na hata wazazi wenyewe walifikiri huelewi. Hawakujali.

Hata hivyo, ambacho hawakujua ni kuwa katika umri huo angalau ulikuwa na akili za kukufanya ujisikie vibaya kuona hicho ulichokiona kikifanywa mbele yako. Pengine ulilia kuona mama yako akipigwa. Uliogopa kumwona baba yako akifoka mbele yako. Leo unapojaribu kuvuta kumbukumbu hizo huwezi. Lakini akili yako, inayo kumbukumbu sahihi ya mambo hayo. 

Kwa hakika, mambo hayo tuliyokutana nayo tukiwa watoto yanawakilisha maisha yetu ya utotoni. Maisha hayo yanaishi ndani yetu. Ni sehemu ya maisha yetu ya utu uzima. Utoto huo una tabia ya kuibuka mara kwa mara leo hii tukiwa kama watu wazima.

Itaendelea…

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles