Na Derick Milton, Simiyu.
TAASISI ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa Mkoa wa Simiyu, imesema katika kipindi cha miezi mitatu Julai hadi Septemba 2021, taasisi za umma zilizoongoza kulalamikiwa na wananchi ni Mamlaka za Serikali za Mitaa na Idara ya Afya.
Lakini mahakama na jeshi la polisi, malalamiko yameonekana kupungua katika kipindi hiki tofauti na ilivyokuwa nyuma ambapo mamlaka hizo ziliongoza kuwa na malalamiko mengi.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022, leo Novemba 4, 2021, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa, Joshua Msuya amesema kuwa malalamiko juu ya taasisi hiyo yametoka kwa wananchi wenyewe.
Amesema ofisi yake imepokea malalamiko 14 kutoka kwa wananchi yanayoelekezwa katika mamlaka za serikali za mitaa, huku Idara ya Afya malalamiko yakiwa 13.
Ameongeza kuwa mahakama ina lalamiko moja na jeshi la polisi ni malalamiko mawili, ambapo ofisi yake imeanza uchunguzi dhidi ya malalamiko yote ambayo yaliwasilishwa katika chombo hicho.
“Pia TAKUKURU imepokea malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wanalalamikia idara nyingine kama ardhi malalamiko matatu, madini (1), binafsi (4) pamoja na utawala (10),” mmesema Msuya.
“Malalamiko mengine yanazihusu Idara ya Maliasili (1), Ushirika (11), Maendeleo ya Jamii (1), Tasaf (1) Uvuvi (1), Kilimo (3) na fedha (1),” ameeleza Msuya.
Msuya ameeleza kuwa katika kipindi hicho, TAKUKURU wamefanya uchunguzi na ukaguzi kwenye miradi yenye thamani ya sh bilioni 2.3 ikiwamo miradi ya kilimo, maji, pamoja na ujenzi.
“Mapungufu machache ambayo tuliyabaini katika miradi yote hiyo, ambayo yangeweza kusababisha mianya ya rushwa tuliyafanyia kazi kwa kufanya vikao na wadau wa miradi husika pamoja na kutoa elimu kwa lengo la kuondoa mianya hiyo ya rushwa,” amesema Msuya.