29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Taasisi za Serikali zadaiwa Sh bil. 2 za maji

 Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Queen Mlozi.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Queen Mlozi.

Na ODACE RWIMO-TABORA

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Tabora (TUWASA) inazidai taasisi mbalimbali za Serikali Sh bilioni 2.5, ikiwa ni malimbikizo ya ankra za maji ambazo hazijalipwa kwa muda mrefu.

Akizungumza juzi katika mkutano maalumu wa wadau wa maji uliofanyika katika Ukumbi wa Mtemi Isike Mwana Kiyungi mjini Tabora, Mjumbe wa Bodi ya TUWASA, John Mchele alisema kitendo cha taasisi za serikali kuendelea kukaa kimya pasipo kulipa malimbikizo ya madeni yao ya ankra za maji kimekuwa kikikwamisha ufanisi wa mamlaka hiyo.

Alizitaja taasisi hizo za serikali zinazodaiwa na mamlaka hiyo kuwa ni Hospitali, Magereza, Jeshi la Wananchi, Polisi na nyinginezo huku akibainisha kuwa ni aibu kwa taasisi nyeti kama hizo kutolipa madeni yao kwani zinapunguza weledi wa TUWASA katika kuhudumia wateja wake.

“TUWASA inadai zaidi ya Sh bilioni 2.5 kama malimbikizo ya madeni ya Ankara kiasi hiki kingelipwa kingesaidia kujiendesha na kuleta ufanisi mkubwa kwetu, lakini sasa tunakabiliwa na changamoto mbalimbali na fedha zipo kwa wateja wetu,” alisema.

Mchele aliitaka TUWASA kuchukua hatua za makusudi za kuwakumbusha wadaiwa sugu wote kulipa madeni yao ili  huduma hiyo iendelee kutolewa kwa wananchi wote.

“Uongozi wa TUWASA naomba msiwe na kigugumizi cha kudai madeni hayo, Rais Dk. John Magufuli akilisikia hili hatafurahishwa nalo kabisa, haiwezekani ofisi za uma ndio ziwe kinara wa kutolipia huduma wanazopewa,” aliongeza.

Mchele alimwomba Rais Magufuli kuziagiza taasisi zote za serikali kulipa malimbikizo ya madeni yao yote wanayodaiwa na TUWASA na wadau wengineo wa maendeleo ili kuboresha huduma zinazotolewa.

Mwenyekiti wa mkutano huo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Queen Mlozi alipongeza jitihada nzuri zinazofanywa na TUWASA katika kuboresha huduma za maji kwa watumiaji wake na miundombinu yake.

Alisema dhamira ya serikali ya awamu ya 5 ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa kila sekta ikiwemo watumishi wote kutekeleza  wajibu wao kwa weledi mkubwa pasipo kuzembea, aidha aliuagiza uongozi wa Mamlaka hiyo kufuatilia wadeni wote ili walipe malimbikizo ya madeni yao.

Mkurugenzi wa TUWASA, Mkama Bwire alikiri mamlaka hiyo kukabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo malimbikizo ya madeni kwa taasisi za serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles