27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

TAASISI ZA FEDHA ZIBADILI MTAZAMO KUHUSU MIKOPO

Na Mwandishi Wetu


MCHANGO wa taasisi za fedha umekuwa ukilalamikiwa kila kukicha kutokana na kuwa umekaa kando na kuonekana kusaidia watu wachache sana ambao ni wale wenye ukwasi mkubwa na wameshindwa kwa ujumla  kumleta mtu mbele waliyemsaidia akiwa masikini hadi kufanikiwa.

Taasisi za fedha na hasa benki zimeshindwa kufuta msemo uliozoeleka kuwa mabenki ni kwa matajiri tu na si kwa wale ambao hawana kitu ikiwamo mawazo mazuri ya biashara kwa kukosa uelewa wa mwenendo wa uchumi na kuishi kwa mazoea.

Hivi karibuni Serikali kupitia Naibu Waziri wa Kilimo, Dk. Mary Mwanjelwa, amesema masharti magumu yaliyowekwa na taasisi za kifedha nchini kwenye mikopo yanasababisha Mtanzania mwenye hali ya chini, kushindwa kunufaika na fursa zilizopo na hivyo kuzitaka taasisi hizo nchini kubadili mfumo wa utoaji mikopo ili iwanufaishe Watanzania wote bila ubaguzi.

Dk. Mary amesema kwa uchungu alipozungumza na wanawake kutoka kata mbalimbali za Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, kwa kudai kuwa

miongoni mwa wanaohitaji mikopo, lakini wamekuwa wakiikosa ni vikundi vya wanawake, ambavyo kila vinapothubutu vinajikuta vinagonga mwamba na kukatishwa tamaa.

Alisema miongoni mwa masharti magumu yaliyowekwa na taasisi nyingi  zikiwa benki ni riba kubwa, sambamba na muda mfupi wa kurejesha mikopo hiyo na kutozingatia  hali halisi ya mambo ikiwamo kilimo amabacho ni cha msimu na hadi sasa hakina bima ya kutofanya vizuri.

Si vizuri kwa taasisi kujiwekea riba ya asilimia 30 au 27, sasa unajiuliza hivi kwa riba hiyo Mtanzania wa kawaida anawezaje kukopa.

“Hii ndiyo sababu inayosababisha Watanzania wengi kutonufaika na mikopo ya benki zetu na badala yake, benki zimebaki kuendelea kuwa taasisi za kuhudumia watu wachache na hivyo kuwanyima fursa wanawake na vijana ambao kimsingi hawana mitaji ya maana ingawa ndiyo nguvu kazi ya nchi ya uzalishaji.”

Anasema inatakiwa ifike mahali benki zimsaidie Mtanzania wa kawaida naye aweze kupata unafuu wa maisha kwa kumsaidia kupitia utoaji mikopo ambayo ni chachu ya kuamsha ndoto za wajasiriamali na kufikia malengo yao.

Wachunguzi wa mambo wanasema mabenki Tanzania yanajikanganya kwani wakati taasisi za fedha zinawasifu wanawake wajasiriamali kwa kurudisha mikopo kwa asilimia 99, lakini mabenki yanakua mazito kutoa mikopo kwa kuwa na hisia potofu kwa kuweka mbele sana dhamana ya mali zisizohamishika (collateral) kwa mikopo hiyo.

“Ni mtazamo wa kihafidhina ndio unaoua mabenki nchini kwa kutozingatia mabadiliko ya mwenendo wa binadamu katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia,” anasema mchumi Habi Litaunga na kuongeza kwani mwekezaji mzuri ni yule anayewekeza kwa baadaye (future) na si kwa yaliyopita  na kuongeza kuwanyanyapaa wanawake na vijana ni kuishi maisha ya kale na kusahau kuwa wapo akina Zukerberg wa Facebook na Jacqueline  Mkindi wa Tanzania Horticulture Association (TAHA) au Dk. Elizabeth Kilili wa Grace  Natural Products Vipodozi ambao wamezuka na sasa matajiri kwa ajili ya kuwezeshwa na si kukatishwa tamaa na mabenki.

Wajuzi wa mambo wanadai wakati umefika kwa Gavana mpya Profesa Florens Luoga, kuweka ulazima wa kila benki kuwa na itifaki ya mikopo kwa kuzingatia makundi yaliyoko pembezoni  mwa jamii na wakulima ili kuleta maendeleo ya kweli na kusisitiza mikopo iwe kwa kiasi kikubwa ya mali badala ya fedha taslimu ili kuzuia kubadilisha matumizi yake ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles