JUDITH NYANGE
TAASISI ya Utafiti na Udhibiti wa Viuatilifu Tanzania (TPRI) imeshauriwa kubainisha dawa ya kuuwa wadudu wa mazao ambayo haina madhara kwa binadamu.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mbegu za Mazao ya Kibo, Francis Chenge, alisema hatua hiyo itawaqwezesha wakulima kuitumia ikizingatiwa wengi hawana elimu ya matumizi sahihi dawa hizo.
Pia aliitaka TPRI a kuwa makini na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika mikoa ya pembezoni mwa nchi.
Alisema zipo baadhi ya dawa za kuua wadudu ambazo hazijakaguliwa na kuthibitishwa na mamlaka husika lakini huingizwa nchini kwa njia za magendo na kusababisha madhara kwa binadamu.
Alikuwa akizungumza kwenye maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa yaliyomalzika juzi katika viwanja vya Nyamong’holo wilayani Ilemela, Mwanza.
Chenge alisema baadhi ya dawa za kuua wadudu wamazao zinaweza kuchangia magonjwa mbalimbali ikiwamo saratani hivyo ni vema TPRI ikabainisha dawa ambazo hazina madhara kwa binadamu.
Alisema ni vizuri pia kampuni za kutengeneza dawa zisizo na madhara kwa binadamu ambazo mkulima atakaa muda mfupi baada ya kupuliza kwenye mazao yake aweze kuvuna kutumia mazao yake kwa chakula au kuyapeleka sokoni .
“Kuna baadhi ya dawa mkulima anatakiwa kukaa saa 24, siku saba au hata mwezi mmoja baada ya kupuliza kwenye mazao aweze kuyatumia kwa chakula na kusiwepo na athari zozote.
“Wakulima wengi hawana elimu kuhusu matumizi sahihi ya dawa hivyo nashauri dawa zenye madhara na zisizo na madhara kwa binadamu zibainishwe ili tahadhari ichukuliwe,” alisema Chenge.
Mkulima kutoka Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, Emmanuel Mgeta, alisema dawa za kuua wadudu wa mazao zina utaratibu wa matumizi yake na mara nyingi huwa zinaandikwa mtumiaji asome maelekezo ya matumizi yake anapoitumia itumie kwa usahihi.
Alisema baadhi yawafanyabiashara huwauzia wakulima dawa ambazo si sahihi kwa kuhitaji tu kuuza kwa sababu amekaa nayo muda mrefu sokoni.
Alisema dawa kama hiyo inaweza kupulizwa kwenye mazao na kuua hata wale wadudu ambao rafiki wa zao husika badala ya wale waharibifu.
Mgeta alisema changamoto iliyopo ni wauzaji wengi wa pembejeo za kilimo kutokuwa na uelewa kuhusu dawa wanazoziuza.
Mara nyingi wengine hawana utaalamu kuhusu biashara hiyo na kushindwa kabisa kumpatia mteja maelekezo anaponunua bidhaa, alisema .