Taasisi yaikabidhi Serikali Simanjiro miundombinu ya shule

  0
  380

  Mohamed Hamad, Simanjiro

  Serikali wilayani Simanjiro mkoani Manyara, imekabidhiwa miundombinu ya Shule ya Msingi Kimelok Kijiji cha Kimotorok, ambayo ni madarasa, nyumba ya walimu, matundu ya vyoo 32 na madawati.

  Miundombinu hiyo iliyojengwa na Asasi ya ECLAT Foundation kwa thamani ya zaidi ya Sh milioni 120, imekabidhiwa jana na Mwenyekiti wa Asasi hiyo, Peter Toima.

  Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zefania Chaula amesema misaada hiyo imekuja wakati mwafaka ambapo kuna mahitaji makubwa kwa wanafunzi na walimu wao.

  “Serikali tuna jukumu la kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi, yanapojitokeza mashirika haya hatuna budi kuipokea misaada hii kwa mikono miwili, kwani tusingeweza kutatua kero zote za wananchi kwa wakati kutokana na kuhudumia wananchi katika maeneo tofauti,” amesema.

  Kuhusu wanafunzi kuishi mbali na shule, mkuu huyo wa wilaya alisema Serikali ina mkakati wa kujenga mabweni kupunguza adha hiyo huku akitaka Serikali ya Kijiji nayo ihakikishe miundombinu hiyo inalindwa sanjari na kuongeza madawati kwa wanafunzi hao.

  Akikabidhi miundombinu hiyo, Mwenyekiti huyo amesema kwa kushirikiana na Shirika la Upendo la Ujerumani, wamefanikiwa kujenga madarasa tisa na kukarabati mengine, ununuzi wa madawati, vyoo viwili vyenye jumla ya matundu 32 na nyumba ya kuishi walimu wawili

  “Matundu 16 ya vyoo yanahudumia wanafunzi wa kike 320 kwa uwiano wa tundu moja watoto 20, wavulana matundu 16 yenye uwiano wa tundu moja watoto 25, ambayo yanapunguza adha ya wanafunzi kwenda kujisaidia porini,” amesema. 

  Awali Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro, Zuwena Omary, alisema wanafunzi hao wana changamoto ya  kutembea Km 30 kwenda na kurudi huku kukiwa na wanyama wakali wanapokwenda na kurudi nyumbani kwao.

  “Mkuu wa Wilaya pamoja na mambo mengine amepata taarifa kuwa wanafunzi hao wana changamoto ya kutoka umbali mrefu, Km 30 tena wakiwa wadogo, hivyo wanashindwa kufika shule kwa wakati na wengine kuwa na ruhusa maalumu kufika  shule kutokana na hali hiyo”

  Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Thomas Masawe amesema, eneo hilo lina wanyama wakali kama vile nyati na chui, jambo ambalo linawalazimu kuahirisha vipindi kwa wanafunzi kusubiri wengine ambao wanatoka mbali kuwa na muda maalumu wa kufika shuleni hapo.

  LEAVE A REPLY

  Please enter your comment!
  Please enter your name here