Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo iliyopo Mongolandege Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetoa misaada ya vyakula na kuwalipia bima ya afya watoto 50 wanaoishi katika mazingira magumu Mtaa wa Viwege katika Kata ya Majohe.
Bima za afya zimetolewa kwa watoto 12 huku misaada mingine ikijumuisha unga, mchele, sukari, mafuta ya kupikia, sabuni, madaftari, mabegi, nguo na viatu.
Akizungumza jana wakati wa kukabidhi misaada hiyo Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Neema Mchau, amesema kupitia shule ya awali wanayoisimamia ya Fahari Day Care Centre waliwashirikisha wazazi na walezi ambao waliwaunga mkono kwa kununua vitu mbalimbali vya kuwapelekea watoto hao.
Aidha amesema walimu wa Fahari Day Care Centre nao walishirikiana kumlipia mtoto mmoja bima ya afya kati ya watoto 12.
“Tunahitaji kuonyesha upendo kwenye jamii yetu kwa kuwa tunaamini sisi wenyewe Watanzania tunaweza kusaidiana tusisubiri wafadhili kutoka nje, na tunaamini unapomfundisha mtoto mdogo juu ya upendo naye atakuwa na upendo na tutafanikiwa kuwasaidia watu ambao hawajiwezi katika jamii zetu. Lengo ni kuhakikisha kwamba tunamuunga mkono mama yetu mpendwa mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tukiamini kabisa kwa pamoja tutakwenda kuijenga Tanzania yetu,” amesema Mchau.
Naye Mwenyekiti wa taasisi ya Tumaini Post Test inayojihusisha kupambana na vitendo vya kikatili katika jamii, Adelhelima Ngonyani, amesema watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu wanakabiliwa na changamoto nyingi na kwamba hii ni mara ya nne kupokea msaada kutoka katika shirika hilo.
“Naishukuru taasisi ya Fahari kwa sababu imeona umuhimu wa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuwasaidia, ninapokwama huwa nawaomba msaada na wamekuwa wakinisaidia,” amesema Ngonyani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Viwege, Amina Kapundi, ameshukuru kwa msaada huo na kusema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikijitoa mara kwa mara kusaidia watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu na kuomba wadau wengine kujitokeza kuwasaidia.