Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Taasisi ya Alkhaibar Haji&Umraah, imewasafirisha mahujaji 16 wanaokwenda Makka kwa ajili ya ibada ya hijja.
Mahujaji hao wameondoka leo saa tisa alfajiri katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA).
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mahujaji hao kuondoka, Mwenyekiti Msaidizi wa Taasisi hiyo, Khalid Sinani, amesema mahujaji hao watapewa huduma zote wakiwa huko na wanatarajiwa kurudi nchini Septemba 7, mwaka huu.
“Kila anayeenda hijja amelipia Dola za Marekani 3,800 ikiwa ni kwa ajili ya mahitaji yote yakiwamo chakula, mahema katika viwanja vitakatifu vya Makka na Arafa.
“Lakini mahujaji hawa pia wametoka maeneo mbalimbali ambapo kati yao kuna wanaume tisa na wanawake nane,” amesema.
Aidha, Khalid amesema wamesafirisha mahujaji wachache kutokana na mazingira lakini walichofanya ni kutoa huduma na si biashara.
“Tunawatoa hofu Watanzania, taasisi hii ipo kwa ajili ya kusaidia Watanzania, mkombozi wa wanaokwenda katika ibada hiyo,” amesema.