23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

TAA NYEKUNDU: MAKONDA ATAJA MAJINA MAPYA 65

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

IKIWA ni siku sita tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alipotaja majina ya baadhi ya wasanii, akiwamo Wema Sepetu na askari polisi aliodai wanahusika na dawa za kulevya, jana ametaja watu 65 wakiwamo wanasiasa na watu wengine maarufu, akiwataka wafike Kituo cha Polisi cha Kati wakajadiliane juu ya tuhuma hizo.

Orodha hiyo mpya ya Makonda ambayo inaweza kutafsiriwa kuwa ni taa nyekundu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini, imekuja ikiwa ni mwaka mmoja na miezi mitatu tangu Rais Dk. John Magufuli kuhutubia Bunge na kuahidi kupambana na wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo.

Pia hivi karibuni wakati akimwapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, alitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuingia katika vita hiyo na kuhakikisha kila anayehusika anakamatwa bila kujali umaarufu wake.

  Novemba 20 mwaka 2015, wakati akifungua Bunge alisema: “Madawa ya kulevya yamekuwa ni janga kubwa kwa taifa letu na kundi linaloathrika zaidi ni vijana wote, wa kiume na wa kike, familia nyingi zimeathirika na nguvu kazi za taifa zimepotea, tutashughulikia mtandao huu unaojihusiaha na dawa za kulevya bila ajizi.

“Tutawatafuta wale wakubwa wanaojihusisha na madawa ya kulevya badala ya kushughulika na dagaa, na ninaposema nasema kweli, naomba Bunge mnisaidie Mungu anilinde na muendelee kuniombea.”

Februari 6, mwaka huu Rais Magufuli alisema: “Shika yeyote peleka mahakamani na ndiyo maana nazungumza, hakuna cha umaarufu, mkishika hawa wote wanaovuta madawa ya kulevya wataeleza nani aliwauzia na huyo aliyewauzia mkimshika atawaeleza ameyapata wapi na huyo naye mkimshika ataeleza ameyapata wapi, lazima mtengeneze hiyo ‘chain’ yote ya kuhakikisha wanaohusika na madawa ya kulevya wanashughulikiwa kikamilifu.

“Vita hii ya madawa ya kulevya hakuna cha mtu aliye maarufu, hakuna mwanasiasa, hakuna askari, hakuna waziri au mtoto wa fulani ambaye akijihusisha aachwe, hata angekuwa mke wangu hapa Janeth, akijihusisha shika, peleka.”

Jana katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam, Makonda alitaja majina ya watu 65 wanaotuhumiwa kwa namna moja au nyingine kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, wakiwamo Kiongozi wa Kambi ya Rasmi ya Upinzania Bungeni, Freeman Mbowe, Mbunge wa zamani wa Kinondoni, Idd Azan Zungu, mfanyabiashara Yusuph Manji na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Alitaja pia wamiliki wa maeneo ya kuchezea kamari (Casino) na wamiliki wa kampuni za nishati ya mafuta na wafanyabishara wengine, ambao wametakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam Ijumaa saa tano asubuhi.  

Hata hivyo, kwenye orodha ya majina aliyokuwa akisoma Makonda, jina la  54 lilisomeka ‘Philemon Mbowe’ ingawa yeye wakati akilitaja alisema ni Freeman Aikaeli Mbowe, Mbunge wa Hai, huku pia jina la Boss Chizenga likijirudia mara mbili (namba 19 na 50).

AMBAO HAWAJARIPOTI

Kuhusu watu ambao hawajaripoti polisi licha ya kutakiwa kufanya hivyo, alisema kama wakigoma au kujificha watapanga utaratibu wa kuwatafuta hata kama ni nje ya nchi.

“Wakati natangaza majina wiki iliyopita kuna wengine walikuwa nje ya Dar es Salaam na wengine wako Afrika Kusini, China na Marekani, walinipigia simu na wako ambao wameshatoa taarifa kwamba watafika. Kitendo cha kukimbia kinatuonyesha kwamba taarifa tulizonazo ni za kweli,” alisema.

Katika hatua nyingine, Makonda alisema Mkurugenzi wa Redio EFM, Francis Ciza, maarufu kama Dj Majjizo, anashikiliwa na polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.

UHALALI WA MALI ZAKE

Alipoulizwa kuhusu uhalali wa mali zake, Makonda alijibu: “Huyo aliyetoa tuhuma amezitoa kwa Spika, kwa hiyo mtapata majibu kwa Spika.

“Kule bungeni wakati mwingine huwa wanachoka wanasinzia, hivyo lazima awepo mtu wa kuwachangamsha, kwa hiyo hizo ni mbwembwe tu.

“Na katika mapambano haya hakuna mtu wa kumrudisha Rais Magufuli nyuma, habari zingine hizi zinasaidia tu kuongeza hamasa ya mapambano ya dawa za kulevya kwa sababu umaarufu pekee tunaoutafuta ni ule wa kutimiza kusudi la Mungu.”

Kuhusu suala la msanii Agnes maarufu kama Masogange kutokamatwa hadi sasa, alisema polisi bado wanaendelea na uchunguzi.

Pia alivitaka vyombo vya habari kuiunga mkono Serikali pale panapokuwa na ajenda ya kitaifa.

“Tukianza kuvutanavutana tutapoteza lengo la msingi la kuwaokoa watoto wetu, inawezekana akaguswa ndugu yako, lakini huu ni wakati wa kufunga mkanda. Tusikatishane tamaa kwa sababu tukishindwa hatakuwa ameshindwa Makonda au Rais Magufuli, bali tutashindwa wote… wewe unayepiga majungu tunakuongezea imani na ujasiri wa kuendelea kuzungumza unachokifahamu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles