31 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

T.B Joshua awafuata Magufuli, Lowassa

mtz1*Atua na msafara wa watu 40

*Afanya nao mazungumzo kwa nyakati tofauti

*Ateta pia na Rais Jakaya Kikwete

*Mugabe, Kagame, Kabila  kutua nchini

 

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WAKATI maandalizi ya kuapishwa Rais mteule Dk. John Magufuli kesho yakiendelea, taifa limeanza kupokea wageni baada ya muhubiri maarufu duniani wa Kanisa la Church of All Nations la nchini Nigeria, T.B Joshua kuwasili jana mchana akiwa na msafara wa watu 40.

Muhubiri huyo aliyewasili Dar es Salaam jana mchana akitumia ndege binafsi, alilakiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na Dk. Magufuli, aliyeambatana na mkewe, Janeth Magufuli pamoja na mtoto wake wa kiume.

T.B Joshua amekuja kushuhudia kuapishwa kwa Dk. Magufuli katika sherehe zitakazofanyika kesho Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuwasili kwa muhubiri huyo, alikwenda Ikulu kwa ajili ya mazungumzo mafupi na Rais Jakaya Kikwete.

Taarifa iliyotolewa Ikulu jana, ilisema kuwa mara baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, T.B Joshua, alikwenda Ikulu moja kwa moja kumsalimia Rais Kikwete na kumpongeza kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu kwa uhuru na amani, huku akiondoka madarakani akiwa mtu mwenye furaha.

“T.B Joshua amempongeza Rais Kikwete pia kwa kumpata Dk. Magufuli kama mrithi wake, akimtaja rais huyo mteule kama rais wa Tanzania wa baraka na fanaka tele katika awamu hii mpya,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.

Muda mfupi baada ya muhubiri huyo kuwasili  nchini, picha zake zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Baadhi ya picha hizo ni zile zilizomuonyesha akiwa uwanja wa ndege na msafara wake pamoja na na Dk. Magufuli na mkewe.

Nyingine zilimuonyesha akiwa ameketi ndani akiwa na Dk. Magufuli na mkewe pamoja na mtoto mdogo wa kiume wa rais huyo mteule.

Dk. Magufuli ni kati ya wanasiasa wa Tanzania waliowahi kwenda nchi Nigeria kwenye kanisa la muhubiri huyo ambaye ni maarufu kwa kutabiri mambo mbalimbali ya kimataifa.

Katika safari hiyo ya Dk. Magufuli nchini Nigeria, aliambatana na mkewe na mtoto wake huyo mdogo wa kiume, ambapo pamoja na kufanyiwa maombi, pia alifanya mazungumzo ya faragha na muhubiri huyo wa kimataifa anayeheshimiwa duniani kwa kuwa na waumini wengi.

Mbali na Dk. Magufuli mwanasiasa mwingine aliyewahi kwenda katika kanisa la T.B Joshua na kufanyiwa maombi ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye aligombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Pamoja na viongozi hao, pia Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alikwenda nchini Nigeria katika maombi.

 

AMTEMBELEA LOWASSA

Mhubiri huyo wa kimataifa mwenye heshima duniani, jana baada ya kutoka Ikulu, alikwenda kumtembelea Lowassa nyumbani kwake Masaki na kufanya naye mazungumzo.

 

MIKASA KANISANI

Septemba 13, mwaka jana watu zaidi ya 100 walifariki dunia mjini Lagos, Nigeria baada ya jengo moja linalohusishwa na T.B Joshua kuanguka.

Taarifa zilieleza kuwa miili kadhaa ilitolewa katika vifusi vya jengo hilo.

Shirika la kusimamia dharura nchini humo, NEMA, lilisema kuwa jengo hilo ni la nyumba za kulala za wanachama wa kanisa la All Nations katika Wilaya ya Ikotun.

Maelfu ya watu mara nyingi uhudhuria maombi yanayoongozwa na T.B Joshua kwa kuwa wanavutiwa na uwezo wake wa kuwaponya watu.

Alipohojiwa T.B Joshua kuhusu ajali hiyo ya kuanguka kwa jengo hilo, aliomba radhi kwa walichokifanya waumini wake kwa waokozi na waliokuwa wakirekodi tukio hilo.

Waumini hao walikuwa wakiwazuia waokozi na waliokuwa wakirekodi tukio hilo kufanya kazi yao.

 

HISTORIA YAKE

Nabii Temitope Balogun Joshua au maarufu kama T.B. Joshua, alizaliwa Juni 12, mwaka 1963 nchini Nigeria.

T.B. Joshua amekuwa kiongozi wa kanisa kubwa nchini Nigeria lijulikanalo kama The Synagogue, Church of All Nations (SCOAN) ambalo pia linaendesha kituo cha televisheni cha Emmannuel TV.

Mtumishi  huyo wa huduma za kiroho amehusika katika miujiza mingi na maelfu ya watu wamefunguliwa na kupokea uponyaji kutokana na huduma yake.

 

UMAARUFU WAKE

Nabii T.B Joshua ametokea kujitwalia umaarufu sana katika nchi nyingi za Afrika, Ulaya na Asia kwa kutabiri mambo mbalimbali ambayo baadae yalikuwa yakitokea kweli na kuripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari vikubwa na vinavyoheshimika duniani.

Amewahi kutunukiwa nishani kama Officer of the Order of the Federal Republic (OFR) kutoka kwa Serikali ya Nigeria mwaka 2008 na pia aliwahi kuchaguliwa kuwa Mtu wa Karne toka kabila la Yoruba nchini Nigeria ambapo alipewa wadhifa huo na Pan-Yoruba Media Outlet Irohin-Odua.

Na pia anatajwa kama tajiri namba tatu nchini Nigeria.

Nabii T.B. Joshua pia amewahi kutambulika kama mmoja kati ya watu 50 toka Afrika wenye nguvu ya ushawishi kwa jamii na Pan-African Magazine iliyomtaja pia kama mmoja wa watu maarufu sana duniani.

 

UTAJIRI WAKE

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, T.B. Joshua anatajwa kuwa na waumini na mashabiki wapatao milioni 1.5.

Baadhi ya mamia ya video zake zilizopo kwenye mtandao wa Youtube ziliwahi kuleta utata duniani kutokana na mambo aliyowahi kutabiri na kusababisha mamilioni ya watu kuzitafuta kwenye mitandao.

Jarida maarufu la FORBES mwaka 2011 lilimtaja Nabii T.B. Joshua kuwa anashika nafasi ya tatu katika wachungaji matajiri zaidi nchini Nigeria akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni 10 hadi 15.

 

MARAIS KUHUDIA KUAPISHWAJI WA JPM

Wakati huohuo, viongozi wa takribani mataifa 40 wanatarajia kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais mteule Dk. Magufuli, wakiwamo Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe na Paul Kagame wa Rwanda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Kimatiafa, ilieleza kuwa viongozi wengine wataokuhudhuria sherehe hizo ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Jacob Zuma (Afrika Kusini), Joseph Kabila (DRC), Uhuru Kenyatta (Kenya), Filipe Nyusi (Msumbiji) na Edgar Lungu (Zambia).

Taarifa hiyo ilieleza kuwa nchi ya Malawi itawakilishwa na Makamu wa Rais, Saulos Chilima huku Namibia ikiwakilishwa na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, Netumbo Nandi-Ndaitwah na Jamhuri ya Watu wa China itawakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Tawala.

Vilevile nchi nyingine ambazo zimethibitisha kushiriki na zitawakilishwa na kati ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika au Balozi ni pamoja na Burundi, Comoro, Angola, Botswana, Lesotho, Madagascar na Mauritius.

Nyingine ni Norway, Oman, Sudan Kusini, Sweden, Umoja wa Falme za Kiarabu, Marekani, Uingereza, Shelisheli, Swaziland, Algeria, Misri, Benin, Denmark, Ethiopia, Finland, Ufaransa, Ghana, India, Japan, Kuwait, Uholanzi na Nigeria.

Taarifa hiyo ilisema wakuu wa mashirika ya kimataifa na kikanda waliothibitisha kushiriki au kutuma wawakilishi wao ni Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya (EU) na Jumuiya ya Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles