SURA ZIPI KUCHUANA URAIS RWANDA?

0
470
Rais Paul Kagame

NA MWANDISHI WETU,

MCHUANO wa kuwania kiti cha Urais nchini Rwanda umezidi kupamba moto. Ni  mwezi mmoja tu umebaki kabla ya Wanyarwanda kuamua nani wa kuliongoza Taifa hilo.

Joto la kisiasa linazidi kushika kasi kutoka kwa wapambe, wafuasi, mashabiki na watu mbalimbali kutoka nje na ndani ya nchi hiyo. Watu wengi wanatazama ni mwanasiasa gani mwenye ubavu wa kumwangusha Paul Kagame. Nani anaweza kuutupa nje utawala wa chama cha RPF? Ni kina nani wanaogombea urais?

Uamuzi wa NEC

Juni 27 ilikuwa siku ya kutangaza majina ya wagombea waliokidhi vigezo vya kuwania Urais wa Rwanda. Tume ya Uchaguzi nchini Rwanda (NEC), imemwidhinisha Rais Paul Kagame kutoka Chama cha RPF na Frank Habineza kutoka Chama cha Democratic Green Party of Rwanda (DGP) kuwania Urais nchini humo ifikapo Agosti 4, mwaka huu.

Uchambuzi wa majina ya wagombea uliofanywa na Tume ya Uchaguzi ulianza Juni 12 hadi 23, mwaka huu, hatimaye Juni 27, kutangazwa wanasiasa hao wawili wa awali ambao wamekidhi vigezo vya kupigiwa kura katika kinyang’anyiro cha urais.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Profesa Kalisa Mbanda, ametangaza baada ya wawili hao kukidhi vigezo vyote vinavyohitajika kikatiba.

Hata hivyo, Mbanda amesema wagombea binafsi wameshindwa kukidhi vigezo vyote kuruhusiwa kuwania wadhifa huo.

Wapewa siku tano

Tume hiyo sasa iliwapa siku tano wagombea hao kuhakikisha kuwa wanatimiza vigezo hivyo, vinginevyo watazuiwa kushiriki katika uchaguzi huo. Hii ina maana ifikapo Julai 5 ndiyo siku ya mwisho ya wagombea hao kutimiza matakwa ya NEC kisha watatangazwa kama wamekidhi vigezo au la.

Kigezo ambacho hawakutimiza ni kutopata sahihi za wapigakura 600 kutoka kwa wilaya 12 kati ya 30 nchini humo. Wagombea hao ni pamoja na Gilbert Mwenedata, Diane Shima Rwigara, Philippe Mpayimana na Fred Sekikubo Barafinda.

Tume imewapa hadi Julai 5, mwaka huu waweze kuwasilisha sahihi hizo kabla ya kutangaza orodha ya mwisho ya wagombea urais siku mbili baadaye yaani Julai 7.

Wagombea binafsi wamekuwa wakilalamikia kusumbuliwa na maofisa wa usalama katika harakati zao za kujitambulisha kwa raia wa nchi hiyo na kueleza mipango yao iwapo watachaguliwa kuongoza nchi hiyo.

Yuko wapi Askofu Nahimana?

Askofu wa zamani wa Kanisa Katoliki ni miongoni mwa waliotangaza mapema sana kugombea urais wa Rwanda mwaka huu, lakini amekuwa kimya kabisa.

Joseph Nahimana ni kasisi wa zamani wa Kikatoliki ambaye aligusa mioyo ya wananchi wa Rwanda ambao walifikiria atakuwa na jipya kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, hata hivyo jina lake halionekani.

Kwa muda mrefu askofu huyo amekuwa akiishi ughaibuni, lakini aliamua kurudi Rwanda. Kimsingi alianza kukumbana na vikwazo vya kurejea Rwanda  baada ya kukataliwa kuingia nchini humo Desemba mwaka jana.

Juhudi zake za kurejea nchini Rwanda zilikuwa na lengo la kuandikisha chama chake na kugombea akiwa na wenzake watatu.

Askofu huyo alikutana na vikwazo vya kuingia nchini Rwanda walipokuwa mjini Nairobi nchini Kenya kuelekea Rwanda kutoka nchini Ufaransa anakoishi kama mkimbizi.

Serikali ya Rwanda haikutaka kuzungumza lolote kuhusu tukio hilo wakati huo, lakini Mashirika ya Rwanda yanayotetea masilahi ya majeruhi wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 walikuwa wameanza kulalamika kuwa akamatwe kwa madai kwamba tovuti yake inaendeleza na kuchochea fikra za mauaji ya kimbari. Hadi leo haifahamiki yuko wapi.

Paul Kagame (RPF)

Anagombea kipindi cha tatu cha urais. Amekaa madarakani kwa miaka 17. Kagame alianza kuongoza Rwanda kama ‘kaimu’ rais mwaka 2000 baadaye mwaka 2003 na 2010 alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo. Hata hivyo, alianza vita vya madaraka toka mwaka 1994 akiwa anaongoza kikosi cha waasi cha RPF.

Phillipe Mpayimana

Huyu ni miongoni mwa wagombea ambao hawakutimiza kigezo cha kupata sahihi za wapigakura 600 kutoka kwa wilaya 12 kati ya 30 nchini humo.

Alitangaza kuombea urais mapema Februari mwaka huu. Kitaaluma ni mwandishi wa habari ambaye aliishi katika kipindi cha vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.

Mpayimana mwenye umri wa miaka 46, sasa amekuwa akifanya kazi na mashirika mbalimbali ya kutoa misaada.

Maisha yake toka wakati wa mauaji ya kimbari amekuwa akiishi katika nchi za Ufaransa na Ubelgiji. Je, jina lake litarudi NEC na kupitishwa?

Diane Shima Rwigara

Ni mgombea binafsi, lakini hajakidhi vigezo vya NEC ya Rwanda hivyo anatakiwa kuendelea na utaratibu wa kutafuta wadhamini 600 katika mikoa mbalimbali kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.

Binti huyo mwenye umri wa miaka 35, amesisitiza kuwa mkakati wake wa kwanza ni kuhakikisha anapambana na umasikini uliotamalaki nchini humo.

Licha ya picha zake chafu kusambazwa mitandaoni, bado Diane hajakata tamaa na ameelezea nia yake ya kumwondoa madarakani Paul kagame. Je, jina lake litarudi NEC na kupitishwa?

Frank Habienza

Huyu ni mgombea pekee kutoka chama cha upinzani ambaye amekidhi vigezo vya Tume ya uchaguzi nchini humo. Frank Habineza kutoka Chama cha Democratic Green Party of Rwanda ametangazwa mapema wiki hii kukidhi vigezo vinavyohitajika, hivyo atachuana kwenye kinyang’anyiro cha urais Agosti 4, mwaka huu. Je, wananchi wa Rwanda watampa nafasi ya kuwa rais wao?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here