32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

SUMAYE: VYAMA VIKONGWE HAVILETI MAENDELEO

KAMPENI: Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu wakimnadi mgombea ubunge wa chama hicho Jimbo la Ukonga,Asia Msangi(katikati) katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mzambarauni, Dar es Salaam jana. PICHA SILVAN KIWALE

Na AZIZA MASOUD -Dar es Salaam


WAZIRI Mkuu mstaafu ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye, amesema nchi ambazo hazitawaliwi na vyama vilivyopigania uhuru, ndizo zenye maendeleo kuliko zinazotawaliwa na vyama vilivyopigania uhuru kwa sababu vikiendelea kukaa madarakani vinakuwa na viburi.

Sumaye alitoa kauli hiyo jana katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mzambarauni wakati wa ufunguzi wa kampeni za mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga kwa tiketi ya Chadema, Asia Msangi.

“CCM ina kiburi na hii ni tabia ya haya machama yanayojidai yameleta uhuru, yana kiburi sijawahi kuona ndiyo maana nchi za Afrika zenye maendeleo ni zile zilizoondoa vyama kongwe madarakani, mnaona  Kenya kuna Kanu leo? Hata ukiangalia nchi nyingine zinazoondelea hakuna maendeleo yaliyoletwa na vyama vilivyopigania uhuru,” alisema Sumaye.

Alisema vyama vikongwe vilivyopo vinachangia kuwafikisha watu pabaya, hivyo lazima wananchi wachukue hatua kwa kuviondoa madarakani.

“Hawa watu tuna shida wanataka tuishi kama hatuna shida, sisi tumetoka katika vyama tawala tumeacha ulaji, lakini nilikuwa nafikiria nawezaje kuwa na raha wakati wananchi wanaangamia,” alisema Sumaye.

Alisema vyama vya upinzani duniani kote ikiwamo nchi ya Marekani, ndivyo vinavyotetea wanyonge kwakuwa chama kilicho madarakani kinatetea masilahi yake ili kiendelee kubaki madarakani.

“Wakina Heche (Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche) vitu anavyoongea hawawezi kuongea wabunge wa CCM, Waitara alikuwa huku alishindwa kufungua mdomo, sasa hivi kahamia CCM mnafikiri ataweza kuongea?” alisema.

Sumaye pia aliwataka wana CCM kuacha kufanya vitu ambavyo vinaashiria kuua demokrasia nchini kwakuwa kufanya hivyo ni kujiua wao wenyewe.

“Wana CCM hili jambo ambalo wanafanya la kuua demokrasia mnadhani mnaua Chadema, lakini wanajiua wao na wengine, demokrasia ikifa hakutakuwa na amani, wananchi mnapaswa kufahamu wanaoua demokrasia ni adui wa taifa hili.

“Wanaonunua madiwani ni maadui wa taifa hili. Tunaomba demokrasia ipewe nafasi yake na ionekane, chama cha upinzani kipewe haki sawa na chama tawala, nawaambia wana CCM tuache kulinywesha taifa hili sumu ambayo inatuua polepole,” alisema Sumaye.

Alisema vyama ya upinzani vipo kisheria kwa lengo la kuleta upinzani na watu kupata huduma na si kutumia umaskini wa watu ili wandelee kuwaabudu.

Naye Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala, Makongoro Mahanga, alisema njia pekee inayotumiwa na CCM kwa sasa katika uchaguzi ni kuiba kura kupitia mabalozi na kukiri kwamba hata yeye alipokuwa anagombea kupitia chama hicho alikuwa anashinda kwa njia hiyo.

“CCM nawafahamu sana, njia zao za kushinda ni kupitia mabalozi, wanawatumia kununua shahada za kupigia kura, hivyo ndivyo wanavyoshinda, hata mimi walinifanyia hivyo na nikawa nashinda,” alisema Mahanga.

Alisema pamoja na kutumia mbinu hizo, bado wanaona haziwatoshi na kuamua kuanzisha utaratibu wa kuiba kura.

“Hizi mbinu wanazotumia zote wanaona hazitoshi, wamekuja na mbinu za kutuibia kura dakika za mwisho, msikubali kuibiwa kura, hizi kura zinazoibwa ni za kwenu, zilindeni,” alisema Mahanga.

Alisema ameshaongea na marafiki zake waliopo CCM, wamemtaarifu kuwa hawawezi kumpigia kura mgombea wa CCM kwakuwa hawamuhitaji.

Mahanga alisema wanachama wa CCM hawawezi kuweka jambo hilo wazi kwakuwa ni waoga, hivyo wameahidi kumpigia kura mgombea huyo kwa siri.

Aliwataka wakazi wa Ukonga kuhakikisha wanalinda kura zao.

Kwa upande wa mgombea, Asia, aliwaomba wakazi wa Ukonga wampatie kura ili awasaidie kusimamia masuala mbalimbali ya kijamii.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles