Mwandishi Wetu
JANA Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alitangaza kujitoa kuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na kile alichodai kuminywa kwa demokrasia ndani ya chama hicho, hasa pale mwanachama anapotaka kugombea nafasi ya uenyekiti wa taifa ambayo kwa sasa inashikiliwa na Freeman Mbowe.
Sumaye ambaye alijiunga na Chadema kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa lengo la kuimarisha upinzani kama alivyodai, anasema ameamua kuachana na siasa za vyama na vyeo na badala yake yuko huru kuwa mshauri wa chama chochote kitakachohitaji huduma hiyo.
Hatua hii ya Sumaye inazua mjadala si kwake tu bali hata kwa baadhi ya makada waliobaki ndani ya Chadema.
Ndiyo maana kuna maswali kadha wa kadha Chadema wanapaswa kujiuliza kwanini hasa viongozi au wanachama wanaojiunga nao kutoka vyama vingine wanaondoka baada ya muda fulani.
Pia wanapaswa kutambua kwamba wanapopata wanachama wenye sifa za kama Sumaye na Edward Lowassa ambao wana rekodi ya kufanya kazi za utumishi wa umma kwa nyadhifa kubwa ndani ya dola, wanaweza kuwa na mchango mkubwa wa kujenga taasisi yao.
Sifa nyingine ya viongozi wa aina ya Sumaye ni kwamba wanafahamu hata mwenendo wa ndani wa CCM, na sasa wanajua mwenendo wa ndani wa upinzani, hivyo tuliamini wangeweza kutoa mchango mkubwa wa kubadili mfumo wa vyama vya upinzani kutoka siasa za harakati kwenda kwenye siasa za kitaasisi.
Pia kwa upande wa Chadema, kinapaswa kichukue changamoto alizotoa Sumaye na hasa suala la demokrasia ya ndani ya chama hicho na kuzifanyia kazi badala ya kujibishana katika kipindi hiki cha uchaguzi wao wa ndani.
Kwa upande wa Sumaye, uamuzi wake umeonyesha sura mbili. Sura ya kwanza ni ile ya kutaka nyadhifa mbili za uenyekiti kwa wakati mmoja jambo ambalo linatia shaka kwamba hasa lengo lake lilikuwa nini.
Sura ya pili huenda amekosa uvumilivu wa kuhimili mikiki mikiki ya siasa za upinzani, ambayo yeye binafsi amedai kwamba alipoteza baadhi ya stahiki zake.
Kwa maoni yetu, Sumaye ambaye amesema hajiungi na chama kingine cha siasa na badala yake anaweza kutoa ushauri katika chama chochote cha siasa, tunamshauri kwa dhati atumie uzoefu wake wa miaka 10 ya uwaziri mkuu kuanzisha taasisi ya maendeleo ya jamii kama alivyofanya aliyekuwa Rais na bosi wake, Benjamin Mkapa aliyenzisha Mkapa Foundation inayojikita katika kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Tunampa ushauri huo kwa sababu akizingatia uzoefu wake kiungozi na wadhifa mkubwa aliowahi kuhudumu ndani ya nchi, amejikusanyia heshima inayompa uwezo wa kutafuta rasilimali ndani ya nchi na nje ya nchi.
Kwa heshima hiyo, anaweza kuendelea kulisaidia taifa katika sekta za elimu, maji na hata mifugo na kilimo, hivyo kutoa mchango katika juhudi za Serikali kupanua wigo wa ajira kwa vijana kupitia sekta binafsi.
Tunaamini Sumaye anaweza kuisaidia jamii moja kwa moja bila kujihusisha na siasa kwani amehudumu miaka mingi katika siasa.
Mwisho tunadhani Chadema wanapaswa kutumia uchaguzi huu kupeleka ujumbe kwa umma wa Watanzania na dunia kuwa mapambano ya demokrasia wanayoyafanya katika nchi yanaakisiwa na uchaguzi wa ndani kwa sababu malalamiko yoyote yatakayoibuka yanakinyima chama hicho uhalali wa kupambania demokrasia nje.